MAREKANI: WATU wasiofahamika wamevamia katika Kanisa linalotumiwa na watu weusi kwenye Jimbo la Mississippi nchini MarekanI kisha kuliteketeza kwa moto na kuandika maneno yanayosema “Mpigie Kura Trump”.
Kanisa hilo la Hopewell Missionary Baptist linalopatikana eneo la Greenville Mississippi lilijengwa miaka 111 iliyopita.
Msimamizi wa kituo cha zimamoto ameeleza kuwa moto katika kanisa hilo uliwashwa makusudi.
Shambulio hilo limetokea wiki moja kabla ya uchaguzi wa urais kufanyika Jumanne wiki ijayo.
Maafisa wanasema ujumbe ulioandikwa kwenye jumba hilo ni wa kuzua hofu huku Meya wa Greenville, Mississippi akisema kuwa kisa hicho ni cha “chuki na woga” na shambulio la moja kwa moja dhidi ya uhuru wa watu kuabudu”.
Tukio hilo linawakumbusha watu kuhusu visa vya kuchomwa moto kwa makanisa ya watu weusi miaka ya 1950 na 1960, watu weusi waliokuwa wanapigania haki zao.
Maafisa wa FBI wakishirikiana na wachunguzi wa jinai wa Jimbo la Mississippi kwa sasa wanaendelea na uchunguzi.

