Fransic Cheka akikagua zana zake kazi.
Na Imelda Mtema |Risasi Jumamosi
Spidi yetu inaendelea kuwa ileile ya 120, kuhakikisha tunakupa kilicho bora kabisa. Ndiyo maana tunajitahidi kila wiki kuvuka boda nje ya Jiji la Dar ili kuwafuata mastaa na wenye majina walio nje ya jiji hili.
Wiki hii, Mpaka Home ilisaga lami hadi Mji Kasoro Bahari. Hapa nazungumzia Morogoro, nyumbani kwa mwanamasumbwi maarufu ndani na nje ya Bongo anayeshikilia Ubingwa wa Uzito wa Kati na wa Juu (WBF). Hapa namzungumzia Fransic Cheka (34), mwenye makazi yake eneo la Kilimahewa hapa Morogoro mjini. Hapa Cheka anaishi na mkewe aitwaye Tosha (30) pamoja na wanaye.
Ni vitu vingi msomaji wangu unaweza ukawa huvijui kuhusu bondia huyu, ungana nami ili upate vingi zaidi.
Anaishi maisha gani yeye na familia yake?
“Maisha yangu ni ya kawaida mno, huwezi kuaamini kama mimi ni bondia mkubwa sana ndani na nje ya nchi na ninayeshikilia mikanda nane, tena niliyopewa baada ya kushinda kila mara, lakini maisha yangu hata ya mtu ambaye siyo maarufu yana afadhali.”
Kipato chake anakipataje? Ni kwa ubondia tu?
“Kwanza mimi mara ya mwisho nilipigana Februari, mwaka huu. Sasa kama ningekuwa ninategemea ngumi tu, si familia ingekufa njaa? Mimi kazi kubwa niliyokuwa naitegemea ni ya kuokota makopo na chupa tupu lakini sasa hivi nimesimama kidogo kwa sababu ya matatizo niliyoyapata ya kufungwa hivyo ninamtegemea zaidi mke wangu ambaye ana kiduka chake ndiyo kinatusaidia kutupa riziki ya kila siku.”
Ngumi zake za ulingoni anazileta kwa mkewe?
“Hapana, naanzaje kumpiga mke wangu ngumi za ulingoni? Mke wangu ni mtu mwenye busara zake. Siyo kwamba nakataa kwamba hakuna mifarakano, ipo na ukizingatia mimi na mke wangu, tuna miaka 16 sasa kwenye ndoa. Kwa hiyo tumekuwa kama ndugu, tunapogombana, tunaweka mambo sawa, maisha yanaendelea.”
Anamsaidia mkewe kazi za nyumbani au analeta uanaume?
“Ukweli mimi ninaweza kuwa tofauti na wanaume wengine. Kwanza sina aibu kwenye suala la kumsaidia mke wangu kazi za nyumbani kama kufua, kukaa na watoto na kuchota maji na kama ni kuniroga, basi mke wangu kaniroga kizungu, sipindui kwake.”
Mlo wake vipi? Ni wa kibondia?
“Mlo wangu siyo wa kutisha sana, hata mke wangu anaweza kukuambia, napendelea ugali wa dona na uji wake na kuna wakati namuomba mke wangu anipikie ugali asubuhi, nikipata mlo huo naweza kushinda bila kula maana kwenye ngumi uhitajiki kilo nyingi hivyo nakula kwa mahesabu.”
Ni faida gani aliyoipata kwenye ubondia?
“Faida ninayoweza kusema nimepata labda ni hela kidogo kwenye upiganaji ngumi, nikaongezea na hela za kuokota chupa ndiyo nikaweza kujenga lakini karibia nyumba tatu nilizojenga, hela kubwa ni ya chupa na nyingine za mke wangu anazofanyia biashara, maana kwenye ngumi ni kujulikana tu na si kingine.”
Anatumia usafiri gani?
“Sina usafiri binafsi. Mara nyingi ninakodi bodaboda lakini sehemu ambayo ninaweza kutembea, huwa natembea kwa miguu na wenye magari yao wananipita.”
Ana watoto wangapi na angependa warithi kazi yake ya ubondia?
“Mimi nina watoto wawili, History (9) na Azenga (mwaka mmoja na nusu). Sitaki hata mmoja aje kuwa bondia, kazi ninayotaka waje kufanya ni hii ya kuokota chupa ambapo mpaka sasa hivi nimewafundisha wakiona chupa wanaziokota, wanaweka sehemu moja lakini ubondia sitaki kabisa maana wataumizwa na faida wasipate.”
Pambano lipi alipata fedha nyingi?
“Tangu nimeanza kupigana, pambano nililopata fedha nyingi ni lile nililopigana na marehemu Thomas Mashali. Nakumbuka nililipwa shilingi milioni kumi na ukiangalia mabondia wengi wanapata fedha nyingi wanapopigana na mimi.”
Vipi bado anatumikia kifungo cha nje?
“Ndiyo, ratiba yangu ya kila siku asubuhi lazima nifanye usafi na Mungu akipenda labda mwakani Januari ndiyo ninaweza kumaliza kifungo changu ambacho kimeweka maisha yangu pabaya sana.”
Ana kitu gani ambacho watu hawakifahamu?
“Najua hiki kitu wengi hawakifahamu, mimi ni Mmakonde kuna nyama moja nzuri sana naipenda ya Panya Buku, wale wakubwa tena waliobanikwa, nikienda Mtwara siwezi kuondoka bila kula.”
Tuzo alizopata zina maana gani kwake?
“Nina tuzo tatu ambazo ni muhimu sana kwangu. Kuna Tuzo ya Kikwete, kwa ajili ya mashabiki wangu. Kuna Tuzo ya TASWA, kwa ajili ya wafungwa na waokota makopo wote na tuzo nyingine ni kwa ajili ya familia yangu kwa mchango mkubwa sana kwangu hasa mke wangu Tosha.”
Mkewe huwa anakwenda kumuona ulingoni anapopigana?
“Mara nyingi sana anakuwepo ninapopigana na ni jasiri hata ninaposhindwa mchezo siku hiyo ananipa moyo kuonesha kuwa mbona mapambano mengine ninapopigana huwa ninashida!”
Ana mpango wa kupigana hivi karibuni?
“Ndiyo, natarajia kupanda ulingoni Desemba 17, mwaka huu nchini India ambapo nitapambana na Vijenger Singh ndiyo maana sasa hivi nipo kambini kwa ajili ya kujifua, lakini mimi pia nimeandaa pambano kama promota ambapo Cosmas Cheka (mdogo wake) na Mkenya watapigana pamoja na mabondia wengine. Pambano hilo litafanyika Desemba 9, mwaka huu hapahapa Morogoro kwenye Ukumbi wa Mango Garden.”
HAYA NDIO MAISHA HALISI YA FRANCIS CHEKA

