×

Polisi Wavamia Ofisi za Jamii Media, Wafanya Upekuzi na Kuchukua Wafanyakazi 2 kwa Mahojiano

jamii-forumDAR ES SALAAM: Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam  jana Desemba 15, 2016, lilivamia ofisi za mtandao wa Jamii Forums (JF) na kufanya upekuzi na  kuondoka  na  nyaraka za usajili wa Jamii Media ikiwemo cheti cha mlipa kodi, cheti cha BRELA, leseni ya biashara na nyingine.
Askari hao walivamia ofisi hizo jana mchana wakiwa wamefuatana  na  na Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao  huo, Maxence Melo, wakafanya  upekuzi na kuwahoji baadhi ya wafanyakazi.
Baada ya kufanya upekuzi ndani ya ofisi hiyo walielekea nyumbani kwa mkurugenzi huyo,  kufanya upekuzi kabla ya kumrudisha  rumande kwa vile hakufikishwa mahakamani.
Melo alikamatwa  juzi  na   kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi  ambako aliwekwa selo.
Anakabiliwa na mashtaka ya kuzuia upelelezi wa makosa ya mtandao kwa kushindwa kutoa taarifa binafsi za watumiaji wa mtandao wa Jamii Forums ambazo polisi walizihitaji.
Taarifa iliyotolewa jana na mtandao huo iliwataka watumiaji wake kutokuwa na hofu yoyote na kwamba Jamii Forums haina server Tanzania wala Africa .
“Tunaomba umma utambue kwamba Jamii Media haina servers wala min-server ofisini kwake, nchini Tanzania wala Afrika. Pili, tunaomba watumiaji wa JamiiForums.com wasitiwe wasiwasi juu ya usalama wa taarifa zao. 
“Teknolojia tunayoitumia (encryption) kumsajili mtumiaji wa JamiiForums.com haituwezeshi kumfahamu mtumiaji yeyote labda yeye akubali kwa hiari yake kujiweka wazi mtandaoni.” Ilieleza taarifa hiyo.
Awali ilielezwa kuwa angefikishwa mahakamani jana Jumatano, lakini haikuwa hivyo.
=======
TAARIFA ILIYOTOLEWA NA JAMII MEDIA

Leo mida ya mchana, polisi kutoka kituo cha Kati, Dar es salaam wakiambatana na Mkurugenzi mtendaji wa Jamii Media, Ndugu Maxence Melo, walifika katika ofisi za Jamii Media kwa ajili ya ukaguzi.

Zoezi hilo limekwenda sambamba na kuwahoji wafanyakazi (Social Media Engagers na Content Quality Controllers) juu ya utendaji wa shughuli zao za kila siku.
Baada ya ukaguzi na mahojiano, polisi wameondoka na nyaraka za usajili wa Jamii Media ikiwemo cheti cha mlipa kodi, cheti cha BRELA, leseni ya biashara, n.k.

Pia polisi imewachukua wafanyakazi wawili kwa mahojiano zaidi.

Polisi wameelekea nyumbani kwa Maxence Melo ambako nako wamefanya ukaguzi ndani ya nyumba. Katika zoezi zima la ukaguzi, sehemu zote mbili, Jeshi la Polisi halikuhitaji wala kuchukua kifaa cha mawasiliano ya kimtandao kama router, flash, hard disc, au kompyuta.

Msafara umeelekea Polisi kituo cha kati kukamilisha mahojiano kati ya Mkurugenzi na wafanyakazi wawili waliochukuliwa.

Tunaomba umma utambue kwamba Jamii Media haina servers wala min-server ofisini kwake, nchini Tanzania wala Afrika. Pili, tunaomba watumiaji wa JamiiForums.com wasitiwe wasiwasi juu ya usalama wa taarifa zao. Teknolojia tunayoitumia (encryption) kumsajili mtumiaji wa JamiiForums.com haituwezeshi kumfahamu mtumiaji yeyote labda yeye akubali kwa hiari yake kujiweka wazi mtandaoni.

Imetolewa na Uongozi,
Jamii Media.

halotel-strip-1-1

Saida Karoli: Diamond Plutnumz Atapeliwa (Exclusive Interview)