GAMBIA: JUMUIYA ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) imeiteuwa Senegal kuwa nchi itakayoongoza hatua za kijeshi kumuondoa madarakani rais wa Gambia, Yahya Jammeh ikiwa atakataa kung’atuka wakati kipindi chake kitakapofika tamati mnamo Janauri 19, mwakani.
“Vikosi vya kijeshi viko tayari kuwapa watu matakwa yao, ikiwa wapatanishi wanaoongozwa na rais wa Nigeria Muhammadu Buhari watashindwa kumshawishi bwana Jammeh kuachia madaraka, alisema Marcel Alain de Souza ambaye ni kiongozi kwenye jumuiya hiyo.
Ameongeza kuwa si matarajio ya Ecowas kuwasha moto au kuishambulia Gambia ikiwa bwana Jammeh anawapenda watu wake, inabidi aondoke madarakani.
Awali Jammeh alikubali kushindwa na mfanyabiashara Adama Barrow wakati wa uchaguzi uliofanyika Disemba 1, mwaka huu na kumpigia simu mshindi akimpongeza, lakini baadaye akaagiza kubadilishwa kwa matokeo akidai kuwa kulikuw na udanganyifu.
