RAIS Rodrigo Duterte wa Philippine ametishia kuwasaka mafisadi serikalini na kuwadondosha kutoka kwenye helikopta ikiwa angani, jambo ambalo amesema aliwahi kulifanya.
Akizungumza huko Camarines Sur kaskazini mwa Philippines juzi (Jumanne), Duterte alisema aliwahi kumsukumia nje ya helikopta mtu aliyekuwa amemteka mtu mwingine ambapo mtu huyo (mtekaji) alikufa. Rais huyo alisema hayo akizungumza na gazeti la Philippine Star kwamba alifanya hivyo wakati akiwa meya wa Jiji la Davao, ambapo kilichofanyika ni helikopta kupaa juu zaidi kisha kumdondosha mtu huyo.
“Kama wewe ni fisadi, nitakuchukua katika helikopta na kukusukumia nje ikiwa angani wakati nakwenda Manila,” gazeti hilo linamkariri akisema huko Tagalog ambapo aliongeza: “Nimewahi kufanya hivyo, kwa nini nisifanye tena?”
Duterte alikuwa Camarines Sur baada ya kutembelea maeneo yaliyokumbwa na kimbunge kilichoitwa Typhoon Nock-Ten, kilicholipiga eneo hilo Siku ya Krismasi.
Baada ya kutangaza misaada ya fedha kwa waathirika wa kimbunga hicho, alisisitiza kwamba kuupiga vita ufisadi kutakuwa kipaumbele cha majukumu yake ya kipindi cha miaka sita madarakani, ikiwa ni pamoja na kupiga vita madawa ya kulevya ambapo watu zaidi ya 6,000 wameuawa katika tafrani za biashara hiyo.
Duterte anajulikana kwa kauli zake za ajabu. Kuna wakati aliwahi kusema alitamani awe mtu “wa kwanza” katika kundi lililombaka mfanyakazi wa kidini kutoka Australia katika vurugu za gerezani mwaka 1989. Pia aliwahi kusema angewaua wanaye iwapo wangetumia madawa ya kulevya. Mwanzoni mwa mwezi huu , Duterte alikiri kuua watu watatu yeye mwenyewe.
Mawaziri wa Duterte kila mara huelezea kauli hizo kama utani au mafumbo. Hata hivyo, tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeitaka Philippines kufanya uchunguzi wa mauaji yaliyodaiwa kufanywa na Duterte.