UTURUKI: Takriban watu 39 wakiwemo wageni 15 wanahofiwa kuuawa na wengine 69 kujeruhiwa katika shambulio la klabu ya burudani mjini Istanbul nchini Uturuki.
Akitoa taarifa hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Waziri huyo Süleyman Soylu amesema kuwa mtu aliyekuwa amejihami kwa bunduki aliwafyatulia risasi watu waliokuwa wakijiburudisha katika mkahawa huo wa Reina majira ya saa 7:00 usiku wakati ambapo watu walikuwa wakisherehekea kuukaribisha mwaka mpya 2017.

Mtu huyo aliingia katika klabu hiyo akijifanya kikaragosi kilichovaa mavazi ya Santa Claus na punde kuanza kuwafyatulia risasi kiholela waliokuwepo. Baadhi yao iliwabidi kujirusha baharini kuepuka msusuru wa risasi zilizokuwa zinafyatulia.

Polisi mmoja ni miongoni mwa waliofariki. Huku waliojeruhiwa wakikimbizwa hospitali, maafisa wa usalama wanaendelea kufanya upekuzi katika eneo hilo lakini muhusika wa shambilo hilo hajakamatwa bado.