×

PM Majaliwa: Walimu 4,000 wa Sayansi na Hisabati Kuajiriwa

  majaliwa-3
  Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

DAR ES SALAAM: Serikali imesema ipo kwenye mchakato wa kuajiri walimu 4000 wa masomo ya Sayansi na Hisabati.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwa katika ziara yake ya kutembela wilaya mpya za jiji hilo, akianzia na Kigamboni siku ya leo.

Majaliwa amesema mchakato wa ajira hizo unaendelea chini ya Ofisi ya Rais Utumishi, na muda wowote kutoka sasa mchakato huo utakapokamilika, majina yatatolewa na walimu hao kuajiriwa.

Kuhusu walimu wa masomo mengine, Waziri Mkuu amesema walimu wa masomo mengine hususani ya sanaa wapo wa kutosha na kwamba wanapaswa kusubiri kwakuwa wao wako wengi zaidi na hakuna uhaba na uhitaji wa walimu hao wa masomo ya sanaa.

Hivi karibuni, Wizara ya Elimu iliwataka wahitimu wa ualimu katika masomo ya sayansi na hisabati kutuma taarifa (CV) zao ili izihakiki kabla ya ajira, mchakato ambao tayari umekamilika na majina yalitumwa katika wizara ya utumishi.