×

‘Bomu’ Lazua Taharuki Kiwanda cha Nondo Dar

bomu

Lango kuu la kiwanda cha nondo palipokuwa na taharuki ya ‘bomu’.

DAR ES SALAAM: KITU kinachodhaniwa kuwa bomu kimezua taharuki miongoni mwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Nondo kilichopo maeneo ya Mwenge-ITV jijini Dar es Salaam baada ya kukutwa katika lundo la vyuma chakavu kiwandani hapo.

Baada ya taarifa hizi kuufikia mtandao huu, waandishi wetu bila kuchelewa walifika katika kiwanda hicho na kubahatika kuingia ndani kwa kuruhusiwa na walinzi wa kiwanda hicho waliokuwa getini.

Baada ya kufika ndani, waandishi wetu walikutana na maofisa wa polisi, askari waliovalia sare za trafiki na askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) ambapo mmoja wa maofisa wa polisi aliwauliza waandishi wetu kilichowapeleka humo na nani aliyewapa taarifa.

Waandishi wetu walijitambulisha kisha kueleza kuwa walizipata taarifa hizo kutoka kwenye vyanzo mbalimbali, lakini majibu hayo hayakuwaridhisha ambapo mmoja wa maofisa hao alimsukuma mwandishi wetu mmoja aliyekuwa karibu naye na kumtaka atoke nje kisha akafunga geti.

Waandishi waliondoka eneo la tukio huku wakiambulia picha ya geti la kiwanda hicho pasipo kupata taarifa kamili kutoka katika uongozi wa kiwanda hicho.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Suzan Kaganda, kuhusiana na tukio hilo, alisema taarifa hizo zilikuwa hazijamfikia.

DENIS MTIMA NA KASMIR MSELECHE /GPL