×

Mtego Wamkamatisha Mhadhiri wa Chuo Kikuu kwa Rushwa ya Ngono

takukuru-kinondoniDAR ES SALAAM: Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Taifa cha Usifirishaji (NIT) amekamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni baada ya kunaswa katika mtego wa rushwa ya ngono.

Mhadhiri huyo anayefahamika kwa jina la Samson Jovin Mahimbo (66) mkazi wa Makongo Juu, Dar es Salaam alikamatwa jana Januari 12, 2017 katika nyumba ya kulala wageni ijulikanayo kama Camp David iliyopo eneo la Mlalakua, Mwenge jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni, Denis Manumbu (Pichani) amesema kuwa, Samson Mahimbo alikamatwa baada ya kuwekewa mtego kufuatia taarifa iliyotolewa na mwanafunzi huyo aliyeombwa rushwa ili aweze kumpatia alama (marks) nzuri  katika mtihani wake wa marudio (supplementary examination) alioufanya tarehe 5 Januari 2017.

“Bwana Mahimbo alimtaka mtoa taarifa (Mwanafunzi) kufika katika Bar ya Shani iliyoko maeneo ya Sinza jirani na Bar ya Meeda na alitii agizo hilo ambapo walikutana na akapewa majibu ya mtihani wa somo la Road Transport, na kuyaandika ili arekebishe mtihani wake alioufanya Janury 5, 2017”

Baada ya marekebisho hayo mtuhumiwa pamoja na mtoa taarifa walielekea katika nyumba ya kulala wageni ya Camp David na kuingia katika moja ya vyumba vya nyumba hiyo, wakati akiwa tayari ameshajiandaa kwaajili ya kutekeleza azma yake ya kumuingilia kimwili mtoa taarifa, ndipo alikamatwa na maafisa wa TAKUKURU” – Kaimu Mkuu wa TAKUKURU

Mtuhumiwa huyo amekamatwa kwa tuhuma za kufanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 25 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2017.