GEITA: Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa na viongozi wengine wa chama hicho amekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Geita leo Januari 16, 2017.
Chanzo cha taarifa hiyo kimeeleza kuwa, Lowassa na wenzake alipita kituo cha mabasi cha zamani cha Geita wakitokea mkoani Kagera kwenye ziara kuelekea kwenye kampeni za uchaguzi Kata ya Nkome, ambapo walisimamishwa na wananchi waliokuwepo eneo hilo, baada ya kushuka kwenye gari kwa ajili ya kusalimiana nao, polisi waliwakamata na kuwampeleka Kituo Kikuu cha Polisi Geita.
Mpaka sasa haijaelezwa kosa lililosababisha kukamatwa kwake.
Alipopigiwa simu na Mtandao wa Global Publishers, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, ACP Mponjoli Lotson alisema alikuwa nje ya mji wa Geita, hivyo apewe muda ili afuatilie na kujua sababu.
Updates:
Waziri Mkuu Mstaafu na Mgombea wa Urais 2015 kupitia CHADEMA, Edward Lowassa leo alikamatwa na jeshi la Polisi wakati akiwa anaenda kwenye kampeni za uchaguzi Kata ya Nkome na baadaye aliachiwa huru ambapo taarifa za polisi zinadai kuwa walimzuia kwa sababu za kiusalama.
Kupitia kituo cha Television cha Azam wameripoti habari ya kukamtwa kwa Lowassa ambapo baadhi wa wananchi wameeleza tukio lilivyotokea.
“Tulikuwa kwenye msafara ya kumpokea Lowassa lakini tulipofika hapa stendi wananchi walitaka kuongea na Lowassa, kabla hata hajashuka kwenye gari askari walituvamia wakasema tuondoke moja kwa moja twende kituoni”– shuhuda.
Mbali na hivyo, Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi wanaoandamana kwenda kituo cha polisi baada ya Lowassa kukamatwa.
Aidha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita amesema kuwa hawakuwa wamemkamata Edward Lowassa bali walikuwa wakijadiliana naye kuhusu usalama wake na jamii.