
ENDELEA ILIPOISHIA: Uombaji radhi ulifanyika katika shughuli maalum iliyoandaliwa na viongozi wa Jimbo la East New Britaish na shughuli hiyo ilipewa jina la ‘reconciliation ceremony’ yaani sherehe ya maridhiano na ilifanyika Rabaul, mji mkuu wa jimbo hilo ambalo lina wenyeji ambao ni wala watu.
“Katika kipindi hiki tumeguswa na kitendo kile na tunaomba msamaha na tunaamini leo tunafuta rekodi hii (ya kuuawa kisha kuliwa kwa mchungaji na wenzake),” alisema Gavana wa jimbo hilo, Ratu Isoa Tikoca.
Ulaji wa watu ni kitu cha kawaida kwa watu wa sehemu za South Pacific , kwa mfano, Kisiwa cha Fiji kilikuwa kikijulikana kama Kisiwa cha Wala Watu na madazani ya wamisionari waliuawa eneo hilo na kuliwa na wenyeji wa hapo.

Michael C. Rockefeller
Mchungaji Brown alikuwa anajua kwamba wenyeji wa visiwa vya Papua Newa Guinea ni wala watu. Aliwahi kuandika katika makabrash yake kwamba katika pitapita yake kisiwani humo akihubiri aliwahi kutembelea kijiji kimoja akakuta mifupa 35 ya mataya, viganja vya binadamu ikiwa imebanikwa ikiwa kwenye moja ya vibanda kijijini hapo.
“Mikono ya binadamu iliyookwa niliikuta ikiwa inaning’inizwa katika moja vibanda kijijini, nje kulikuwa na mnazi ambao ulikuwa na alama 76 ambazo wenyeji walituambia kila alama inawakilisha mtu mmoja aliyepikwa nyama yake na kuliwa hapa,” alisema Mchungaji Brown enzi za uhai wake alipokuwa akiwaambia viongozi wa Taasisi ya Royal Geographical Society.
Maneno hayo aliambiwa akiwa hajui kwamba wamisionari wenzake wa dhehebu la Methodist aliokuwa nao, tayari nao wameliwa huko alikowatuma kuhubiri na alipojua, aliingiwa na wasiwasi mkubwa juu ya maisha yake.

“Waliuawa na kuliwa kwa sababu tu, walikuwa wageni na wenyeji waliofanya hivyo hawakuwa na sababu nyingine isipokuwa walikuwa na tamaa ya kula nyama zao na kuchukua baadhi ya mali chache walizokuwa nazo,” aliandika Mchungaji Brown.
Kulitokea vurugu kati ya wenyeji na Wazungu kutoka Ulaya baada ya kitendo cha kuliwa watu hao weupe kwani vijiji kadhaa vilichomwa moto na mitumbwi ya wenyeji iliharibiwa. Makabila kumi ya visiwa hivyo yalilaumiwa kwa kushambulia wazungu na kuwala nyama hasa katika eneo linaloitwa Blanche Bay.
Mchungaji Brown aliandika barua kwa Katibu Mkuu wa London Missionary Society aliandika hivi kabla ya kujua kuwa naye alikuwa akiwindwa aliwe: “ Wenyeji wanatuheshimu kuliko mwanzo, hii ni kwa sababu wanajua haki tuliyonayo inayotuumiza mioyo ya kuwaelimisha.”
Hata hivyo, kuna taarifa kuwa Michael Rockefeller (pichani), aliyekuwa mtoto wa Makamu wa Rais wa Marekani, Nelson Rockefeller mwaka 1961 naye aliuawa na kuliwa nyama yake na watu hao. Ilikuwaje? Fuatilia Jumanne ijayo uone yaliyompata. Itaendelea