×

Credo Mwaipopo: Nilichukua fedha za Yanga Nikatimkia Sweden

credo-mwaipopo

…Credo Mwaipopo

Sweetbert Lukonge |CHAMPIONI

UKIAMBIWA utaje viungo bora hivi sasa katika kikosi cha Yanga, lazima utawataja Mnyarwanda, Haruna Niyonzima pamoja na Mzimbabwe, Thaban Kamusoko. Pia unapaswa kutambua kuwa viungo hao siyo wa kwanza kuonyesha ubora wao uwanjani wakiwa na timu hiyo, kwani wamepita viungo wengine machachari klabuni hapo.

Credo Mwaipopo ambaye alijiunga na timu hiyo msimu wa 2006/07, ni mmoja kati ya viungo wazuri waliowahi kutamba na kikosi hicho kabla ya kuachana nacho na kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine.

Kwa wapenzi na mashabiki wa timu hiyo watakuwa wanamkumbuka vilivyo kiungo huyo kutokana na umahiri wake mkubwa wa kutandaza soka aliokuwa nao uwanjani.

Hakuwa mtu wa mchezomchezo kama wasemavyo vijana wa siku hizi kwani katika kipindi hicho alifanikiwa kuiongoza Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu, msimu wa 2006/07, 2007/08 na 2009/10.

Baadhi ya wachezaji alioshirikiana nao katika kuiongoza Yanga kutwaa mataji hayo ni Fred Mbuna, Abuobakar Mtiro, Wisdom Ndlovu, Hamisi Yussuf, Waziri Mahadhi, Gaudence Mwaikimba, Abuu Ramadhan, Thomas Maurice, Amri Kiemba, Maurice Sunguti, Mrisho Ngassa na Abdi Kassim ‘Babi’.

Hata hivyo, baada ya mafanikio hayo aliamua kuachana na timu hiyo na kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine baada ya mashabiki pamoja na viongozi wa Yanga kumchoka.

Hivi karibuni kiungo huyo amefanya mahojiano na Championi Ijumaa ambapo hapa anafunguka zaidi juu ya maisha yake.

Historia yako kwa ufupi

“Mimi ni mtoto wa tano katika familia yetu ya watoto saba, nimezaliwa hapahapa Dar na nilianza kuvutiwa na soka nikiwa mdogo.

 Wapi ulianzia soka?

“Kwanza watu waelewe kwamba baba yangu ndiye aliyekuwa anacheza soka, kwa hiyo mimi nilipita njia zilezile alizopita yeye japo hakucheza sana na badala yake akajikita kwenye kazi yake ya benki.

“Binafsi nilianza soka rasmi nikiwa darasa la tatu Shule ya Msingi Muhimbili ambapo nilikuwa nacheza timu ya darasa na marafiki zangu walikuwa wananiambia wanapenda ninavyocheza.

“Niliendelea hadi nilipohitimu darasa la saba, nikajiunga na Shule ya Sekondari Air Wing, huko nikasoma mwaka mmoja kabla ya Shule ya Sekondari Jitegemee kunichukua.

 Asoma bure Jitegemee

“Kutokana na uwezo wa kucheza soka niliokuwa nao, pale Jitegemee nilisoma bure yaani sikulipa ada hadi nilipomaliza kidato cha nne na baadaye nikaenda Kenya, baada ya hapo nikasomea masuala la kompyuta (IT), hiyo ilikuwa mwaka 2004.

“Nilipomaliza masomo nchini Kenya nikarudi Dar, nikatua katika kikosi cha Kumbukumbu ya Kinondoni kilichokuwa kinashiriki Ligi Daraja la Kwanza kabla ya kuhamia Kimara ambapo kuna siku tukacheza na Friends Rangers na mimi kuonyesha uwezo ambao ulinifanya nitue kwenye kikosi chao.

“Nikacheza Friends kwa mwaka mmoja kabla ya kuhamia Twiga ambayo meneja wake alikuwa Herry Chibakasa ‘Mzozo’, hapo nikadumu mwaka mmoja.

Atua Yanga, aingia na Kiemba

“Kule Twiga nilikaa kwa mwaka mmoja kisha nikaondoka na kutua Yanga nikiwa sambamba na Amri Kiemba ambaye yeye alitokea Kagera Sugar, nikakaa hapo kwa misimu mitatu kabla ya kuondoka mwaka 2009 tena kwa kutoroka.

Asaini Yanga, atorokea Sweden

“Unajua kwamba nilipokaa Yanga ikafikia muda nikaona kwamba sijisikii kuendelea kucheza tena hapa nyumbani, yaani kila siku Dar, Mbeya na Morogoro, hivyo nikapanga iwe isiwe lazima niondoke.

“Wiki mbili baada ya kusaini mkataba mpya Yanga mwaka 2009, nikatoroka na kutua Sweden ambapo huko nilienda kufanya majaribio tu.

Kally Ongala alihusika kumtoa Yanga

“Wakati naondoka Yanga nilikuwa na mawasiliano na Kally Ongala (sasa ni kocha wa Majimaji), yeye ndiye aliyekuwa kila kitu mpaka mimi natua Sweden,  nilikuwa ninawasiliana naye kwa kipindi kirefu.

“Kwa muda huo Kally alikuwa anacheza timu ya South Valley iliyokuwa inashiriki ligi kuu ya nchi hiyo, hivyo nilivyoenda nikawa nafanya nao majaribio kabla ya kurejea Yanga mwaka 2010.

“Nilirudi Tanzania kwa sababu kule muda wa usajili ulikuwa bado, nilipotua hapa kuna baadhi ya mashabiki wakaniambia nibakie hapahapa lakini nikagoma na mwaka huohuo nikarejea Sweden kujiunga na timu ya daraja la pili ya Panlioni IF ambayo nilicheza kwa muda mfupi kabla ya mwaka 2011 kuvunjika mguu.

Akaa nje mwaka mzima, atua kwa Wajeshi

“Kitendo cha kuvunjika mguu malengo yangu yakaharibika kwani ilinilazimu kukaa nje kwa mwaka mzima na kurejea hapa nchini ambapo mwaka 2012 nikajiunga na JKT Ruvu, napo sikukaa sana, nikarudi tena Sweden.

“Huko nikatua katika timu ya daraja la tatu ambayo ilikuwa inataka kushuka daraja, lakini kwa uwezo wetu na wenzangu kina Shekhan Rashid, Mgaya, Richard na Yusuph wote wakiwa Watanzania tukaibakisha daraja baada ya hapo nikaja tena Tanzania kwa mara nyingine.

Arudi Friends, aikacha, atimkia Sweden

“Kule nilikaa kwa mwaka mmoja kabla ya kuja nchini nikatua Friends Rangers, nikacheza kwa misimu miwili 2014/15 na 2015/16 ambapo nikarejea Sweden kuichezea timu ya Kilimanjaro ambayo ni ya Watanzania na kufanikiwa kuipandisha daraja kutoka Ligi Daraja la Nane kuja la saba ambapo sijui kama nitarejea tena.

 Changamoto ulizokutana nazo Yanga ni zipi?

“Licha ya kuwepo kwa changamoto nyingi lakini kwa upande wangu hazikuniathiri sana sababu kabla ya kukutana nazo nilikuwa naziona kwa watu ambao wameshacheza timu hizo.

“Mtu kama John Mwansasu alinisaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na changamoto hizo zikiwemo za kuzomewa na mashabiki wetu wenyewe.

 Maximo alimbania kuichezea Taifa Stars

“Wakati nacheza soka sikuwahi kuichezea timu ya taifa kwa sababu ya Kocha Mbrazili, Marcio Maximo kwani alikuwa na kikosi chake ambacho hakikuwa kinabadilika hata mara moja, niliishia kucheza timu za vijana tu.

 

Shinda Nyumba Awamu ya Pili Yatikisa Jiji la Dar es Salaam