TUNAENDELEA na mfululizo wa mada ya sumu mwilini ambapo wiki iliyopita tuliona jinsi sumu zinavyojitengeneza mwilini. Tuliona makundi mawili ya sumu, ambayo ni sumu ambazo husababisha madhara yasiyorekebishika ambayo ni ulemavu wa maisha (Irreversible effects) na kundi la pili ni aina za sumu zinazosababisha madhara yanayoweza kurekebishika (Reversible effects).
Pia tulijua kuhusu vyanzo vya sumu mwilini. Vyanzo hivyo ni vile vya kutoka nje ya mwili ambavyo binadamu huvitumia na matokeo yake humuathiri. Sumu nyingine hujitokeza kwa kukosa au kutozingatia maelekezo tunayopewa juu ya utumiaji salama wa dawa za kutibu magonjwa.

Jinsi ya uondoaji wa sumu mwilini
Uondoaji wa sumu mwilini hutegemeana na aina ya sumu yenyewe. Njia ya kwanza ni matumizi ya dawa za kuivunja nguvu ile sumu husika ambapo kitaalamu hujulikana kwa jina la antidote. Hapa ni baada ya uchunguzi kufanyika na kugundua aina ya sumu iliyokuathiri na kisha utapewa dawa kulingana na majibu ya uchunguzi wa kitaalamu.
Njia ya pili inayoweza kutusaidia kuondoa sumu na hasa zile zinazozalishwa mwilini ni matumizi ya vyakula bora, hivi ni vyakula ambavyo kwa asili yake huwa na virutubisho ambavyo huvunjavunja na kuondoa sumu mwilini, vyakula hivi kitaalamu huwa na vitu v in a v y oitwa antio x i dants, ambavyo huulinda mwili dhidi ya kemikali hatarishi zinazozalishwa mwilini.
Virutubisho hivi ni pamoja na Vitamin A, Vitamini C na Vitamini E. Vitamini hizi hupatikana katika mboga za majani na matunda, mfano mchicha, spinachi, karoti, matembele, machungwa, nanasi, maembe, machenza na mafuta ya mimea mfano alizeti.
Ili miili yetu iweze kufanya kazi vizuri na tuendelee kuwa na afya njema, inabidi tuepukane na sumu hizi, pale inapotulazimu zitumike (mfano zebaki, migodini), basi tuzidishe umakini katika kujilinda afya zetu, na pia tubadilishe aina ya maisha au ulaji wa vyakula, matunda na mboga za majani ni walinzi wakubwa sana wa afya zetu.
Makala yameandikwa kwa msaada wa Tanzlife LTD.