×

INSANE (MWENDAWAZIMU)-8

MWANDISHI: NYEMO CHILONGANI

ILIPOISHIA

“Mungu! Siamini kama nakwenda kuwa baba! Naomba umsaidie Miriam ajifungue salama,” alisema Boniface huku akiwa ameikutanisha mikono yake huku akiwa amepiga magoti.

SONGA NAYO

Baada ya miezi minne, Edson na mkewe wakarudi nchini Tanzania. Hakuwa akijisikia sawa kwani bado alikuwa na maumivu makubwa mwilini mwake. Hakuweza kutembea kipindi hicho kwani miguu yake ilivunjika na haikuwezekana kurudishwa katika hali ya kawaida hivyo maisha yake yakawa kwenye kiti cha walemavu.

Moyo wake ulimuuma sana, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea katika maisha yake, wakati mwingine alibaki na kujilaumu kwani yeye ndiye alikuwa chanzo cha kila kitu, kama angetulia na mkewe basi asingeweza kupata tatizo alilokuwa amelipata.

Baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam, waandishi wengi waliokuwa na taarifa za ujio wake wakakusanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Walipomuona, wakamshukuru Mungu lakini wakati mwingine waliona kile alichokipata ndicho alichostahili kwani kwa jinsi alivyomuumiza mkewe, hakutakiwa kuwa hai.

Alikwishaambiwa kwamba asingeweza kupata mtoto tena, si kutokupata tu bali hata kufanya mapenzi na mwanamke yeyote isingewezekana. Hilo lilimuuma, uwanjani hapo alibaki akibubujikwa na machozi tu.

Moyo wake uulikuwa kwenye maumivu makali, kutokana na tamaa yake, matokeo yake mwisho wa siku akajikuta akiwa hana lolote, alijiona kuitwa mwanaume suruali, mwanaume asiyekuwa na uwezo wa kumfanya mwanamke amuheshimu.

Yalikuwa maisha yaliomuumiza mno, aliendelea kuingiza fedha lakini kuingiza fedha pasipo kuwa na uwezo wa kulala na mwanamke halikuwa lolote lile.

Huo ulikuwa muda wa kumjali mumewe, alijua kwamba hakuwa na uwezo wowote wa kufanya mapenzi lakini hakutaka kumuacha, kila siku alikuwa pamoja naye, alimkumbuka msichana Stela lakini hakuwa na jinsi, alitakiwa kusahau kila kitu kilichotokea.

Biashara zao zikaendelea, Rachel ndiye aliyekuwa akisimamia biashara zote za familia. Haikuwa kazi kubwa kwani ilikuwa ni kuwapa amri wale wale waliokuwa wakisimamia kuendelea kama alivyokuwa akiwasimamia mume wake.

Mwaka wa kwanza ukakatika, maisha yaliendelea kama kawaida. Nyusoni mwao, wanapokuwa mbele za watu walionekana kuwa na furaha kubwa na wakati mioyo yao ilikuwa kwenye maumivu makali mno.

Hawakujua ni kwa jinsi gani wangepata mtoto. Nyumba ilikuwa kubwa, wao na wafanyakazi wa ndani. Walipoondoka asubuhi, jinsi nyumba walivyokuwa wakiiacha ndivyo walivyokuwa wakiikuta.

Iliwaumiza mno, walitamani hata kama wangekuwa na mtoto ili watakapoondoka, wakirudi wakute mito ipo chini, rimoti imewekwa kwenye kikombe, cd zipo ukumbini, lakini hilo halikuwezekana.

“Ni jambo linaloniumiza mno mke wangu! Sijajua ni kwa jinsi gani tunaweza kuikabili aibu tuliyokuuwa nayo. Kila mtu ananiuliza kuhusu mtoto, sijajua tufanye nini,” alisema Edson huku akimwangalia mkewe usoni, sura yake ilionekana kuwa na majonzi muda wote.

“Ila natumaini Mungu atatupa mtoto tu! Tuendelee kumuamini katika maisha yetu,” alisema Rachel.

“Unaamini hilo?”
“Asilimia mia moja mume wangu! Bado Mungu anaweza kufanya jambo!” alisema Rachel kwa sauti yake ya chini.

“Sawa! Tuendelee kumuamini!”

Japokuwa Edson hakuwa mtu wa kwenda kanisani, naye akaanza kwenda huko, alimuomba Mungu, alijitoa sana kwa ajili ya watu wengine huku moyo wake ukiwa na lengo la kupata mtoto tu.

Siku ziliendelea kukatika, miezi ikasonga mbele lakini hakukuwa na kitu chochote kilichobadilika. Wote wawili wakakata tamaa na kuamua kupanga mipango ya kumuiba mtoto yeyote yule, wakae naye na kumlea kama mtoto wao.

“Unafikiri ni wazo zuri?” aliuliza Rachel.

“Haina jinsi mke wangu! Inatubidi tufanye hivyo tu, vinginvyo, tutaumbuka,” alisema Rachel.

“Basi tufanye miezi tisa ijayo. Kwa sasa hivi naomba nijifanye nina mimba,” alisema Rachel.

Hilo ndilo walilofanya. Rachel akajifanya ana mimba, akaanza kuweka nguo, kitumbo kikaanza kutuna taratibu na baada ya miezi mitatu, akaongeza nguo zake na kujifanya mimba imekua.

Hakukuwa na mtu aliyeleewa kilichokuwa kikiendelea. Nguo ziliongezeka kila miezi na baada ya miezi tisa, akajifanya kujisikia uchungu na kwenda hospitali. Huko, tayari Edson alikwishafanya mipango, aliwaandaa vijana wake kwa ajili ya kuwatafutia mtoto yeyote ili mmkewe ajifanye kama amejifungua huyo.

Vijana hao walikwishaondoka mpaka mitaa ya Posta Mpya. Walisikia kwamba kulikuwa na mwendawazimu ambaye alijifungua wiki moja iliyopita. Walipofika huko mida kama ya saa moja usiku, kama bahati yao wakamkuta Miriam akiwa na mtoto wake. Walichokifanya ni kumfuata usiku na kumpora mtoto huyo na kukimbia naye.

Watu waliliona tukio hilo ila hawakuweza kuwapata watu hao waliokuwa na pikipiki. Kila mtu alishangaa, hawakuamini kama kungekuwa na mtu ambaye angeweza kufanya kitu kama kile.

“Mungu wangu! Wamemuiba mtoto,” alisikika jamaa mmoja huku akionekana kushangaa. Ghafla, gari moja aina ya Noah likatoka katika eneo hilo na kuanza kuwafukuza watu. Kutokana na watu hao kuwa na pikipiki, hakuweza kuwapata.

****

Boniface hakuamini mara baada ya kusikia sauti ya mtoto ndani ya chumba kile. Akainuka na kuanza kushangilia kiasi kwamba watu wote waliokuwa mahali hapo wakaanza kumshangaa.

Alimshukuru Mungu kwa kuwa hatimaye alifanikiwa kupata mtoto wake wa kwanza kutoka kwa msichana aliyekuwa akimpenda sana kipindi hicho. Akatamani afunguliwe mlango na amwangaliee mtoto wake kwani moyo wake ulikuwa na shauku kubwa mno.

Hakutulia kwenye benchi, muda wote alikuwa akizungukazunguka huku akishangilia. Baada ya dakika fulani Miriam akatolewa katika chumba kile na kupelekwa katika chumba kingine. Alibaki akimwangalia, moyo wake ulimpenda maradufu Miriam kwani alionekana mwanamke mzuri kupitiliza.

Baada ya kuwekwa kwenye chumba kingine na mtoto wake, akaelekea huko na kuanza kumwangalia mtoto huyo. Alikuwa mtoto wa kiume, hakutaka kuchelewa, hapohapo akampa jina lake na kumuita Jackson, jina alilokuwa akilipena tangu zamani.

Japokuwa alikuwa mwendawazimu lakini Miriam alionekana kuwa na furaha tele, alionekana kama kufahamu kilichokuwa kimetokea. Alipopewa mtoto wake, alimwangalia huku akichekacheka tu.

Madaktari hawakutaka awe naye, walichokifanya ni kumchukua na kumuweka sehemu. Boniface akawa baba Jackson, moyo wake ulikuwa na furaha mno, hakutaka kujificha, aliamua kuwaambia madaktari ukweli kwamba yeye ndiye aliyekuwa akihusika na mtoto yule.

Ilikuwa siri ambayo wote kwa pamoja waliahidi kuitunza akiwepo Dk. Fabian. Baada ya kukaa siku mbili hospitalini huku akipata huduma zote muhimu, Miriam akatolewa na kuendelea na maisha yake ya mitaani.

Mtoto alikuwa mikononi mwake, hakutaka kumuona mtu yeyote akimsogelea, alimpenda mtoto huyo kupita kawaida. Boniface hakupenda kabisa Miriam awe na mtoto huyo kwani moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno kwani mtoto wake alitakiwa kupata malezi mzuri na maisha ya kitajiri kama aliyokuwa akiishi.

Alichokifanya, asubuhi mpaka usiku alikuwa akimuachia mtoto yule ila ilipofika saa tatu muda wa kuondoka, alikuwa akimfuata na kumchukua mtoto huyo. Miriam alikuwa mwendawazimu lakini kitu cha ajabu alimzoea sana Boniface, Alipomuhitaji mtoto, alimpa na kuondoka naye, kesho, alikuwa akimrudishia kama kawaida.

Siku ziliendelea kukatika mpaka siku ambayo Boniface akiwa ndani ya ofisi yake akichungulia nje kumwangalia Miriam na mtoto wake, ghafla akawaona watu wakiwa kwenye pikipiki, kwanza akashtuka, hakujua watu hao walikuwa wakina nani na walihitaji nini.

Mwanaume aliyekuwa nyuma, akateremka, akamfuata Miriam na kisha kumpora mtoto aliyekuwa naye, akarudi kwenye pikipiki haraka sana na mwenzake kuondoka mahali hapo.

Boniface akashtuka, hakutaka kubaki ndani ya ofisi yake, akateremka kwenye ngazi harakaharaka, alipofika chini, akaingia ndani ya gari lake na kuliondoa mahali hapo. Aliwaona watu hao kwa mbali lakini hakuweza kuwapata kwani kulikuwa na foleni kubwa ya magari, akajikuta akikwamishwa na magari hayo. Pikipiki hiyo ilipofika maeneo ya Stesheni, ikakata kulia na kutokomea huko kuelekea Mnazi Mmoja.

Je, nini kitaendelea

Tukutane Alhamisi mahali hapa.