Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Emmanuel Mrangu (aliyesimama katikati) akimpatia ufafanuzi wa jambo Kaimu Jaji Mkuu (aliyekaa) Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Katibu Msaidizi Tume ya Utumishi wa Mahakama, Enziel Mtei (aliyesimama) akimweleza jambo la kazi bandani kwake Prof. Juma.
Prof. Juma akifuatilia jambo alipotembelea mabanda hayo.
Naibu Mkurugenzi Ufuatiliaji na Tathmini kutoka banda la Maboresho (Judiciary Reforms), Sebastian Patrick (kushoto) akimfafanulia jambo Kaimu Jaji Mkuu kupitia TV iliyokuwa ukutani.
Trafiki wa kituo cha Polisi cha Selander Bridge jijini Dar es Salaam, CPL Amini (kushoto) akimfafanulia jambo mwananchi aliyefika kwenye banda lao kujua sheria inayohusiana na vifaa wanavyovitumia askari kupima mwendo kasi barabarani.
Mtaalam wa Afya (kushoto) kutoka Shirika la Bima ya Afya (NHIF) akimpima presha mwananchi aliyefika kwenye banda hilo ikiwa ni wiki ya elimu ya sheria.

NA DENIS MTIMA/GPL
KAIMU Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma leo ametembelea mabanda ya Wiki ya Sheria yaliyopo viwanja vya Mnazi Mmoja ambaye shughuli zake zilianza wiki iliyopita na zitafikia kilele kesho ambapo Rais John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Profesa Juma ameunga na wananchi ambao wamekuwa wakitembelea mabanda hayo ili kujifunza na kujionea huduma zinazotolewa hapo. Miongoni mwa mabanda aliyotembelea ni ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Baadhi ya huduma za kisheria zilizokuwa zinazotolewa viwanjani hapo ni pamoja na kujua taratibu za ufunguaji mashauri katika ngazi mbalimbali za mahakama, taratibu za kesi za dhamana, taratibu za rufaa, taratibu za kesi za mirathi ndoa na talaka, taratibu za kupokea na kushughulikia malalamiko na msaada wa kisheria.
Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini mwaka huu yanakuja na kaulimbiu isemayo ‘Umuhimu wa Utoaji Haki kwa Wakati Kuwezesha Ukuaji wa Uchumi’.