×

Nilifanya Mapenzi na Maiti 20 Nitajirike-18

ILIPOISHIA

Wakati nikiwa kwenye usingizi mzito, ghafla nikaanza kuota ndoto moja hivi, ndoto iliyousisimua mwili wangu, sikuamini kile nilichokuwa nikikiona kwenye ndoto ile kingekuja kutokea siku moja katika maisha yangu, nilibaki nikiweweseka kitandani pale huku nikijiuliza swali moja la msingi, je ni kweli nilichokiona kingetokea? Sikuwa na jibu hata kidogo. Ndoto yenyewe ilikuwa hivi…

SONGA NAYO

Nilijiona nikiwa nimesimama mbele ya umati mkubwa, sikujua ilikuwa sehemu gani lakini kwa jinsi ilivyoonekana, ilikuwa ni moja ya sehemu iliyowakutanisha viongozi wengi wa nchi.

Nilikuwa nazungumza juu ya jukwaa, kila mtu alikuwa akiniangalia, walikuwepo watu wa mataifa mbalimbali, Wazungu, Wahindi, Wachina na watu wengine. Nilishangaa, sikuwa nikifahamu lugha ya Kiingereza lakini cha ajabu, mahali hapo nilikuwa nazungumza lugha hiyo kwa ufasaha kabisa.

Wote walikuwa kimya wakiniangalia, walikaa katika viti vyao kwa heshima kubwa, nilikuwa na furaha mno, yaani watu hao, ambao kwa kuwaangalia tu walikuwa wasomi watulie na kunisikiliza mimi, nilikuwa na lipi la maana?

Wakati nikiendelea kuota ndoto hiyo, ghafla katika umati ule alisimama mtoto mmoja, alikuwa kama na miaka miwili, alikuwa akilia sana lakini hakukuwa na mtu aliyejali chochote kile na wala hakukuwa na mtu yeyote aliyemtaka anyamaze.

Nilishtuka kutoka usingizini, nilikuwa katika hali isiyokuwa ya kawaida, niliangalia saa yangu na kugundua tayari ilifika saa moja asubuhi. Nikatoka kitandani na kuanza kujiandaa tayari kwa kuondoka hotelini hapo na kuendelea na safari.

Nilichukua taulo na kwenda bafuni. Kitu cha ajabu kabisa, nilikuta bafu likiwa na ndoo mbili, moja ilikuwa ya bluu na nyingine ilikuwa nyekundu. Usiku wa jana nilipokuwa nimefika, nakumbuka kwamba kulikuwa na ndoo moja tu, ile ya bluu, sasa hii nyekundu ilitoka wapi? Nikahisi labda mhudumu aliingia, ila napo haikuniingia akilini kwa sababu tangu nimeingia, sikutoka na mlango nilifunga kwa ufunguo.

“Unashangaa nini?” niliisikia sauti yangu moyoni mwangu, ilikuwa sauti ya yule mganga.

“Hii ndoo imetoka wapi? Tena ina maji!” niliuliza.

“Hii ndoo tumekuwekea sisi….”
“Ya nini?”
“Tunataka uoge maji hayo, tunakupa nguvu ya kukufanya kuwa mtu mwenye nguvu sana. Umekwishawahi kusikia kuhusu Illumiterant?” aliniuliza mganga yule.

“Hapana! Ndiyo nini?”

“Hiyo ni dini yetu, tuna dini ya tofauti kabisa, tupo hapa duniani kwa ajili ya kumuabudu Lusifa, hakuna kingine, yeye ndiye anatupigania na kutulinda, kwa sababu umehitaji utajiri na kupata, hatuna budi kukuingiza katika dini hii, imetapakaa dunia nzima na itakufanya kuwa na utajiri mkubwa, heshima kila kona,” aliniambia mganga huyo.

Kwanza nikashtuka, sikuamini kama maisha yangu yote, mwisho wa siku ningeingizwa katika dini hiyo ya kumtumikia shetani. Nikawa kama nimepigwa butwaa fulani lakini nilitakiwa kukubaliana na mganga huyo pamoja na dini hiyo mpya ambayo niliingizwa kutokana na tamaa za kidunia.

“Nipo tayari…ila unapozungumzia heshima, unanishangaza, nipata hiyo heshima kivipi?” nilimuuliza, mawasiliano yetu wote yalikuwa ya kimoyomoyo.

“Utakuwa mwanamke mwenye cheo kikubwa sana hapa Tanzania, nitakwambia sehemu ambayo tunaabudia, utakwenda huko, utakuwa ukiabudu kila siku utakazotakiwa kufanya hivyo,” aliniambia na kukubaliana naye.

Nilifanya kama alivyoniambia, nikachukua yale maji yaliyokuwa katika ndoo ile na kuanza kuyaoga, kadiri nilivyokuwa nikijimwagia, nilijisikia kuwa katika hali ya tofauti kabisa, mwili ulikuwa ukisisimka na wakati mwingine niliona kama ukitiwa nguvu.

Nilipomaliza, nikatoka na kuvaa nguo zangu, kilichofuata ni kuondoka hotelini hapo. Njiani, sikuona kitu chochote cha ajabu, nilikuwa kimya muda wote, sikuhitaji kelele, hata redio sikuiwasha.

Nilitumia saa kadhaa nikafika Dar es Salaam ambapo niliendelea na kazi zangu kama kawaida. Biashara zile nilizokuwa nimezifungua, ziliendelea kuniingizia kiasi kikubwa cha fedha mpaka kufikia hatua ya kuhama na kuhamia Mbezi Beach, katika jumba kubwa ambapo pia nilikuwa na harakati za kujenga jumba langu la kisasa maeneo ya Bunju.

Baada ya siku mbili, nakumbuka nilitembelewa na wageni wawili, walikuwa wanaume nadhifu, sikuwahi kuwaona kabla, nilipowakaribisha wakaniambia kwamba walifika hapo kwa ajili ya kwenda nami kanisani. Kwanza nikashangaa, ilikuwaje wanifuate na kunitaka niende nao kanisani na wakati sikuwa nikiwafahamu? Mimi na kanisa wapi na wapi na wakati nilikuwa Muislamu na hata jina langu lilikuwa Zakia?
Wakati najiuliza hayo, nikaisikia sauti ya mganga ikiniambia nifanye kile wanachoniambia watu wale, nikakubaliana nao, nikajiandaa na kuondoka nao mahali hapo.

Ndani ya dakika kadhaa tulifika katika jumba fulani hivi, lilikuwa kubwa mno. Kuna kitu cha ajabu kilitokea, mimi ndiye nilikuwa dereva lakini kama ungeniuliza nilipita njia gani mpaka kufika katika jengo hilo, wala sifahamu chochote kile, yaani nilikuwa mtu niliyeendeshwa na mtu na wakati mimi ndiye nilikuwa dereva.

Watu wale wakanitaka kuteremka, tukafanya hivyo na kuanza kulisogelea jumba lile kubwa lililoandikwa Illumiterant, yaani wenyewe wakiwa na maana ya KANISA LA SHETANI.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumapili hapahapa