×

Mwanzo wa mwisho wangu

Kijana mdogo, Benjamin Semzaba au maarufu zaidi kama Ben, anafikishwa mbele ya mkono wa sheria akikabiliwa na kesi nzito ya mauaji. Baada ya kunguruma kwa kipindi kirefu, hatimaye kesi iliyokuwa inamkabili inaelekea kufika mwisho na hukumu kutolewa.

Ushahidi wote umeshakamilika na hakuna shaka kwamba Ben ndiye aliyeua kwani ukiachilia mbali ushahidi huo, yeye mwenyewe mara kwa mara amekuwa akikiri kwa kinywa chakekufanya mauaji hayo na kilichokuwa kikisubiriwa ilikuwa ni hukumu tu.

Wakati kila mtu akiamini kwamba Ben ameua, Jordan Rwechungura, wakili aliyekuwa akimtetea katika kesi hiyo ambaye ukiachilia mbali kazi yake pia alikuwa rafiki mkubwa wa Ben, waliyecheza pamoja tangu wakiwa watoto wadogo, anakuwa mgumu kuamini kwamba ni kweli rafiki yake huyo ameua.

Historia ya makuzi ya Ben, inamfanya Jordan ahisi kwamba Ben hajaua ila ameamua kukubali kwa sababu ambazo yeye mwenyewe ndiye anayezijua. Jitihada zake za kutaka kuufahamu ukweli ili amnasue rafiki yake huyo kutoka kwenye kitanzi kilichokuwa kinamsubiri, zinagonga mwamba kutokana na Ben kukataa kutoa ushirikiano, muda wote aking’ang’ania kwamba ni yeye ndiye aliyeua.

Hatimaye siku ya hukumu inawadia, Ben akiwa amedhoofika sana na kubadilika kutokana na mateso ya gerezani, anaingizwa mahakamani huku mamia ya watu, wakiwemo waandishi wengi wa habari wakifuatilia kwa umakini kesi hiyo iliyogusa hisia za watu wengi.

Upande wa pili, historia ya maisha ya Ben inaelezwa, tangu akiwa kijana mdogo kabisa, akiishi na mama yake pamoja na wadogo zake, Mtaa wa Maporomoko kwenye mji mdogo wa Tunduma.
Je, nini kitafuatia? Ben atapewa hukumu gani?

SONGA NAYO…
Baada ya kufanya kazi ya kupika vitumbua kwa muda mrefu, mama yake Ben alianza kulalamikia maumivu ya tumbo na kifua. Awali kila mmoja alidhani ni maumivu ya kawaida lakini kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele, ndivyo mwanamke huyo alivyokuwa analalamikia maumivu ya tumbo.

Ikabidi aende hospitali ambapo vipimo vya awali vilionesha kifua chake kimepata madhara kutokana na kuvuta hewa yenye moshi kwa kipindi kirefu. Daktari akamshauri kuepuka kukaa kwenye moto, hilo likawa pigo jingine kwa familia hiyo kwani bila biashara ya vitumbua, hakukuwa na namna nyingine ya kupata fedha.

Kwa kuwa siku zote Ben ndiye aliyekuwa akimuandalia mama yake kila kitu katika shughuli hiyo ya upishi wa vitumbua, na mama yake alishaambiwana daktari kwamba kutokanana hali yake ya kiafya hatakiwi kuendelea na kazi hiyo, ilibidi Ben ndiyo ashike usukani.

Badala ya kuamka saa kumi alfajiri kama ilivyokuwa mwanzo, ilibidi ratiba yake ibadilike, sasa akawa anaamka saa nane za usiku ambapo alikuwa akiandaa mahitaji yote muhimu kisha kuanza shughuli ya kupika vitumbua mpaka saa kumi na mbili alfajiri ndiyo ajiandae kwenda shuleni.

Ilikuwa ni mpaka awahesabie wadogo zake vitumbua na kumgawia kila mmoja idadi yake na kuwakabidhi ndiyo aanze kujiandaa kwenda shule. Ratiba hiyo ilikuwa ngumu mno kwake, siku za mwanzo alikuwa akifika darasani, asubuhi tu anaanza kusinzia na kumfanya ashindwe kuelewa chochote kinachofundishwa.

Jioni akirudi nyumbani, alikuwa hawezi kupumzika mpaka akatembeze kwanza vitumbua vilivyosalia kisha ndiyo arudi nyumbani na kuungana na wadogo zake na mama yao kupata chakula cha usiku.
Kutokana na uchovu wa kutwa nzima, alikuwa akikosa hata muda wa kujisomea, akawa analala mapema ili awahi kuamka saa nane usiku na kuendelea na ratiba zake kama kawaida.

“What’s wrong with you Ben? Why are you always drowsing when im teaching?”
(Ben, unasumbuliwa na nini? Mbona kila nikiingia darasani kufundisha wewe unasinzia?) Madam Joyce aliyekuwa akiwafundisha somo la Kiingereza, alimuuliza Ben asubuhi moja baada ya kugundua kuwa alikuwa akisinzia muda mfupi tu baada ya vipindi kuanza.

“Nothing serious madam, im taking influenza dosage which makes me feel drowsy,” (hakuna jambo kubwa mwalimu, nakunywa dozi ya mafua ndiyo inayonifanya niwe hivi) alijibu Ben huku akikaa vizuri kwenye siti yake. Macho yake yalikuwa yamevimba na kuwa mekundu kiasi kwamba hata mwalimu huyo alimuonea huruma, akampa ruhusa ya kutoka darasani na kwenda kupumzika nyumbani, jambo ambalo Ben hakukubqaliana nalo.

Badala yake, alitoka na kwenda kwenye mabweni ya wanafunzi waliokuwa wanasoma ‘boarding’, akatafuta kitanda kimoja na kujilaza. Kutokana na uchovu aliokuwa nao, alikuja kushtuka wakati kengele ya kuashiria kumalizika kwa vipindi ilipogongwa, akakurupuka na kuchukua madaftari yake na kuungana na wanafunzi wenzake.

Siku hiyo ilipita, ratiba hiyo ikawa inaendelea huku ufanisi wake kwenye masomo ukianza kupungua taratibu. Kiwango chake cha ufaulu kikaanza kushuka, hali iliyowafanya walimu wake wamshutukie na kuanza kumhoji kilichokuwa kinasababisha hali hiyo.
Hata hivyo, mwenyewe hakuwa wazi kueleza kwamba kila siku usiku alikuwa akiamkausiku kwa ajili ya kupika vitumbua ambapo biashara hiyo ndiyo iliyokuwa ikiendesha maisha yao. Suala hilo lilibaki kuwa siri kati yake na familia yake.

Faida kidogo iliyokuwa ikipatikana, ilikuwa ikitumika kununua mahitaji muhimu ya familia hiyo pamoja na dawa za kumtibu mama yao ambaye kadiri siku zilivyokuwa zinasonge mbele ndivyo alivyokuwa anazidi kuteseka.

Licha ya kujitahidi kumpeleka kwenye hospitali mbalimbali za serikali, bado hali ya kiafya ya mama huyo wa familia ilizidi kuwa mbaya. Wakawa wanabadilishiwa dawa mara kwa mara ambazo kutokana na uhaba wa dawa kwenye hospitali za serikali, walilazimika kuwa wanazinunua kwenye maduka ya dawa.
Hata hivyo, kutokana na ughali wa dawa hizo, taratibu mtaji wa vitumbua ulianza kupungua kwani walilazimika kutoa fedha nyingi zaidi ili kugharamia matibabu ya mama yao. Kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele ndivyo mtaji ulivyozidi kupungua na hatimaye ukaanguka kabisa, biashara ya vitumbua ikaishia hapo.

“Sasa tutaishije wanangu?”
“Inabidi nianze kuwa naenda Blaki (Black Market) kufanya vibaua vya kubeba mizigo ya watu wanaonunua bidhaa kwenye maduka na kuzipeleka kwenye stesheni za tazara upande wa Nakonde, Zambia.”
“Inabidi iwe hivyo tu mwanangu, najua unachoka lakini jitahidi, wewe ndiyo kiongozi wa hii familia,” alisema mama yake Ben kwa sauti iliyoonesha kwamba yupo kwenye maumivu makali.
Kesho yake, Ben hakwenda kabisa shuleni na badala yake, alienda kwenye soko maarufu linaloziunganisha nchi mbili za Tanzania na Zambia maarufu kwa jina la Black Market. Akaanza kuomba vibarua vya kubeba bidhaa zilizokuwa zinanunuliwa na wateja, wengi wakiwa ni raia wa nchi ya Zambia na kupeleka mpaka kwenye stesheni ya treni ya Nakonde.

Japokuwa haikuwa kazi nyepesi, Ben alijitahidi kadiri ya uwezo wake, akawa anajikaza kiume na kufanya kazi ngumu tofauti na umri wake kwa lengo al kuhakikisha familia yao inakula na mama yake anapata matibabu.

Mpaka anarudi nyumbani jioni ya siku hiyo, mkononi alikuwana shilingi elfu kumi na sita za Kitanzania pamoja na Kwacha za Zambia ambazo alipozibadilisha kuwa fedha za Kitanzania, jumla zilifika shilingi elfu ishirini na nane.
Akaondoka kurejea nyumbani kwao, mwili mzima akiwa amechafuka kutokana na kazi ngumu alizokuwa akifanya. Alipitia sokoni ambapo alinunua mchele, nusu kilo ya nyama na kumnunuliamama yake dawa za kifua. Akarudi nyumbani alikopokelewa kama mfalme.

Wadogo zake wakamuandalia maji ya kuoga huku utaratibu wa kupika chakula ukianza haraka kwani muda ulikuwa umeenda sana. Mama yake alimshukuru sana kwa ujasiri aliouonesha lakini akamsisitiza kwamba ni muhimu awe anaenda kwanza shsuleni kisha akishatoka ndiyo aendelee na mambo mengine, ushauri ambao aliuoana kuwa wa maana.

Siku hiyoilipita, hayo ndiyo yakawamaisha mapya ya Ben, kila alipokuwa akienda shuleni, alikuwa akibeba pia nguo za kazikwenye begi lake la madaftari. Jioni baada ya kumaliza masomo, alikuwa harudi nyumbani mpaka apitie kwanza kwenye soko hilo na kufanya vibaruia kisha ndiyo arejee nyumbanikwao, akiwa na chochote mkononi.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumamosi kwenye Risasi Jumamosi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave a Comment