×

Ulimwengu azidi kuwadatisha Wazungu

Na Omary Mdose | CHAMPIONI

MSHAMBULIAJI Mtanzania anayekipiga kwenye kikosi cha AFC Eskilstuna ya Sweden, Thomas Ulimwengu, amezidi kuwadatisha Wazungu wa timu hiyo baada ya kuonekana ni mchezaji aliyekamilika kwa kila kitu kwenye idara yake.

Ulimwengu ambaye amejiunga na timu hiyo katika usajili wa dirisha dogo Januari, mwaka huu akitokea TP Mazembe ya DR Congo, amepewa mkataba wa miaka mitatu wenye kipengele cha kuhama kama ikitokea timu nyingine inamhitaji.

Jumanne ya wiki hii, Ulimwengu aliitumikia kwa mara ya kwanza timu yake hiyo kwenye mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya Elfsborg uliopigwa jijini Barcelona, Hispania na kutoka sare ya bao 1-1 huku yeye akitoa pasi iliyozaa bao la kusawazisha lililofungwa na Chidi Dauda Omeje.

Mkurugenzi wa michezo wa timu hiyo, Azad Budak, amemzungumzia Ulimwengu kwa kusema: “Hapa tumepata mchezaji kweli, ana kasi na nguvu, ataongeza kitu kwenye safu yetu ya ushambuliaji.

“Kubwa zaidi ni mzuri pale anapobaki na mpinzani mmoja, mbali na hilo, pia ana uwezo mkubwa wa kucheza kama mshambuliaji na winga zote.”

Shinda Nyumba Awamu ya Pili Yatikisa Jiji la Dar es Salaam