
CHAMPIONI | LIVERPOOL, England
LIVERPOOL awali ilikuwa inapewa nafasi kubwa zaidi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu kutokana na kasi yao.
Kila mmoja alikuwa anaamini kuwa timu hii ni bora na inaweza kutikisa kwenye ligi hiyo na kuwazidi vigogo kadhaa. Mwaka jana bado timu hiyo ilikuwa bora huku wachezaji wake wakionyesha kiwango cha juu sana, lakini tangu kuanza kwa mwaka huu mambo yamekuwa tofauti sana.

Liverpool haijawa timu ile ambayo ilikuwa inapewa nafasi kubwa tena pamoja na kwamba ilifanikiwa kutoka sare ya bao 1-1 na vinara wa ligi, Chelsea.
Liverpool chini ya kocha wao mbishi, Jurgen Klopp, sasa haina matumaini ya kutwaa ubingwa tena, bali dalili nyingi zimekuwa zikionyesha kuwa timu hiyo inataka kufanya kila linalowezekana kumaliza kwenye nafasi nne za juu na siyo ubingwa tena.
Liverpool ambayo mshambuliaji wao Sadio Mane, alirudishwa haraka kuwahi mchezo dhidi ya Chelsea, haijashinda mchezo
wowote wa Ligi Kuu England tangu mwaka huu umeanza, hali uwezo tena wa kupambana na timu nyingine kubwa kwa sasa. Mara ya mwisho kwa timu hiyo kushinda ilikuwa Desemba 31 wakati ilipofanikiwa kuichapa mabao 1-0 timu ya Manchester City.
Timu hiyo haijashinda kwenye michezo kumi mfululizo na bado inaonekana kuwa na michezo mingine migumu inakuja.
Katika wiki tatu zijazo, Liverpool itatakiwa kuhakikisha inarudi kwenye kasi yake wakati itakapozialika timu za Tottenham na Arsenal ambazo ni timu kubwa za juu kwenye Ligi Kuu England.
Ingawa timu hiyo haijapoteza mchezo wowote kila inapokutana na timu kubwa za juu, ambazo ni Manchester United, Manchester City, Totteham Hotspur, Arsenal na Chelsea, lakini inatakiwa kufanya kazi kubwa sana kwenye michezo hiyo ijayo. Inaaminika kuwa kama Liverpool watashinda kwenye michezo hiyo miwili mikubwa basi itakuwa ni nafasi yao kuonyesha mwanga wa kuwania nafasi nne za juu msimu huu.
Ingawa bado hakiwezi kuwa kigezo kikubwa sana kwao kwa kuwa wamekuwa wakipoteza michezo midogo kuliko mikubwa.
Kitendo cha wikiendi iliyopita Klopp kukubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya timu ndogo ya Hull City kimeonyesha kuwa Liverpool haijafanya vizuri kwenye michezo mingi waliyocheza na timu ndogo msimu huu.
Klopp Amebakiza miezi 18 kwenye mkataba wake na Liverpool na inaaminika kuwa mafanikio yake makubwa ambayo anatakiwa kuyapata kwenye timu hiyo ni kutwaa ubingwa tu.
Liverpool ndiyo kati ya timu zile kubwa ukiachana na Spurs ambayo imekuwa ikisubiri ubingwa wa England kwa muda mrefu zaidi kwani mara yao ya mwisho kuutwaa ilikuwa mwaka 1990.
Katika pointi 21 za hivi karibuni,
timu hiyo imefanikiwa kuzoa pointi 13 tu, huku ikiwa imepoteza michezo mitatu dhidi ya timu za mkiani.
“Tumekuwa kwenye wakati mgumu kwa kipindi kifupi kilichopita, lazima tuonyesha kuwa tunapata shida na hali hii ilivyo.
“Kila mmoja anatakiwa kujua kuwa hali yetu kwa sasa siyo nzuri, na kila mmoja anatakiwa kuongeza juhudi
ili tuweze kutoka kwenye hali
hii.
“Siyo matokeo mazuri kama tulivyoanza msimu huu, lakini bado naamini kuwa tunaweza kufanya vizuri zaidi siku zijazo.
“Lazima tujiangalie, lakini ukweli ni kwamba wachezaji wangu hawakwepi hali iliyo kwa sasa.
“Nawajua vijana wangu nimekuwa nao kila siku, lakini nisema kuwa wanatakiwa kutoa matunda mazuri uwanjani, tumetengeneza matatizo mengi.
“Makosa yangu ni makosa yetu, lakini lazima tukubali kuwa tunatakiwa kukubali kila tunapolaumiwa na kuchukua lawama hizo na kusonga mbele zaidi,” alisema Klopp.
Kwa sasa timu hiyo ipo katika nafasi ya tano ikiwa imeshaondoka kwenye timu zile nne za juu hali ambayo inaonyesha wanaweza kuwa na kazi kubwa ya kurejea kwenye nafasi hiyo.
Liverpool ambayo mwezi mmoja nyuma ilikuwa inapewa nafasi ya kutwaa ubingwa wa England kwa sasa ipo nyuma ya vinara Chelsea kwa tofauti ya pointi 13, ambazo zinaonekana nyingi sana kutokana na ligi hiyo kubakiza michezo 13 tu ili imalizike.
Pamoja na kwamba Liverpool hawajafungwa na timu kubwa za juu, lakini wamejikuta wakifungwa na Hull iliyopo katika nafasi ya 18, Burnley iliyopo nafasi ya 12, Swansea ambayo ipo katika nafasi ya 17 na Bournemouth ambayo ipo katika nafasi ya 14 kwenye ligi.
Katika michezo 24, ambayo timu hiyo imecheza hadi sasa imefanikiwa kushinda michezo 13, ikiwa imefungwa mine lakini ikatoka sare kwenye michezo saba ambayo ndiyo imechangia kwa sehemu kubwa timu hiyo kuwa kwenye nafasi hiyo ya tano.
Inaaminika kuwa kocha wa Liverpool, anaweza kuondoka kwenye timu hiyo ikiwa itashindwa kufuzu kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwakani.