NA MWANDISHI WETU | CHAMPIONI | MUNICH, UJERUMAN
STAA wa zamani wa Ujerumani, Michael Ballack amemwambia kiungo wa Arsenal, Mesut Ozil kuwa kama anataka kutwaa makombe ajiunge na Bayern Munich.
Kwa sasa Arsenal wapo nyuma ya vinara Chelsea kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi 12 na hawana matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa huo msimu huu.
Ballack ambaye amefanya vizuri kwa kipindi kirefu akiwa na Bayern amesema huu ndiyo muda wa kiungo huyo kwenda Bayern ili aweze kutwaa makombe makubwa.
Maisha ya Ozil kwenye kikosi cha Arsenal yanalegalega kwa kuwa staa huyo raia wa Ujerumani amebakiza mkataba wa miezi 18 tu kwenye timu hiyo.
Hata hivyo, amewahi kunukuliwa akisema kuwa anafuraha ya kuishi London kama atapewa mkataba ambao mshahara wake ni kuanzia pauni 200,000 kwa wiki.
“Mesut ni mchezaji wa ajabu, anajua kuwa yeye ni staa mkubwa sana kwenye kikosi cha Arsenal.
“Kila klabu itakuwa inataka kumsajili, kwa sasa anaishi London sehemu ambayo ni bora kwake.
“Lakini kwangu naona kama Ozil anataka kutwaa makombe mengi makubwa anaweza kufanikiwa akiwa na Bayern Munich kama atakubali kujiunga nayo,” alisema kiungo huyo wa zamani wa Bayern Munich.