
Rais Magufuli

Wanakwaya wa Gwajima

Gwajima siku aliporipoti polisi kuhojiwa
Siku moja baada ya Askofu Gwajima kuachiliwa kwa dhamana kutoka Kituo Kikuu cha Polisi (Central) alikokuwa akishikiliwa kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya, Rais John Pombe Magufuli amewashukia wanakwaya wa askofu huyo ambao Alhamisi iliyopita, wakati Gwajima alipofika polisi kwa ajili ya kuhojiwa, walikusanyika nje ya kituo cha polisi na kuanza kuimba nyimbo za dini.
Akizungumza kwenye ukumbi wa mikutano, ikulu wakati wa hafla ya kuapishwa makamishna mbalimbali aliowateua hivi karibuni, Rais Magufuli alisema ameshangazwa na tukio hilo, sambamba na tukio la wafuasi wa Yusuf Manji ambao walikuwa wakilifuta gari la kiongozi huyo wa Klabu ya Yanga wakati alipowasili kituoni hapo kuhojiwa, na kueleza kwamba matukio hayo ni dharau kwa jeshi la polisi.
Rais Magufuli akaongeza kwa kumuagiza IGP sambamba na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, kutoruhusu tena matukio kama hayo na yeyote atakayefanya kitendo hicho, atupwe mahabusu bila kujali ni nani.