×

Dakika 180 Zamuibua Mavugo Upya

STORI: NA MWANDISHI WETU | CHAMPIONI | DAR ES SALAAM

LAUDIT Mavugo amegeuka gumzo kubwa kitaa kutokana na mabao yake mawili katika mechi mbili zilizopita, kusaidia kuipa timu yake ya Simba pointi sita muhimu na kukaa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara. Katika mechi hizo mbili ambazo Mavugo alicheza kwa dakika zote 180, kwa maana ya 90 kwa kila mechi, Simba ilifunga jumla ya mabao sita.

Mchezo wa awali dhidi ya Majimaji Februari 4, Mavugo alifunga bao la tatu Simba ikishinda 3-0, mabao mengine yakifungwa na Ibrahim Ajibu na Said Ndemla. Kwenye mchezo wa juzi Jumamosi dhidi ya Prisons, Mavugo alifunga bao la tatu pia katika ushindi wa 3-0, huku mabao mengine yakifungwa na Ibrahim Ajibu na Juma Luizio. Sasa straika huyu ana mabao sita katika chati ya wafungaji. Kabla ya kufunga mabao hayo, Mavugo alikuwa na ukame wa kutofunga katika mechi nyingi.

Mara ya mwisho alikuwa amefunga Oktoba 23, 2016 dhidi ya Toto ambapo Simba ilishinda 3-0. Alikuwa amecheza mechi tisa za ligi kuu bila bao. Katika mchezo wa juzi, Mavugo alikuwa gumzo kwani licha ya kufunga bao, alitengeneza pasi murua ambayo ilizaa bao la pili la Simba lililofungwa na Ibrahim Ajibu. Sasa mashabiki wa timu hiyo wanasubiri kuona kama ataendelea kufunga katika mechi zijazo ikiwemo ile dhidi ya Yanga ambayo itachezwa Februari 25, mwaka huu.

Inadaiwa kuwa siri kubwa ya mafanikio ya Mavugo ni kubadilika kwa mfumo wa Simba. “Nashukuru Mungu kwa ushindi huu ambao tumeupata mfululizo tena wa mabao mengi ambayo yanafungwa na washambuliaji, hakika naona sasa mipango yangu inaanza kufanikiwa.

“Awali baada ya kuona washambuliaji hawafanyi vizuri niliamua kubadili mfumo na kutumia viungo wengi lakini hivi sasa tumebadili tena mfumo na tunaanzisha washambuliaji watatu na wakuwa wakifanya vizuri kama ninavyotaka, hakika kwa hali hii naamini kabisa hata katika mechi zetu zijazo tutafanya vizuri kama tulivyofanya dhidi ya Majimaji pamoja na Prisons.

“Sina hofu yoyote hata tutakapocheza na Yanga ninaamini tutafanya vizuri kutokana na jinsi wachezaji wangu walivyo hisi sasa,” alisema Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog.