

“BABA yangu siku zote alikuwa akinisapoti. Alipenda kuniona nikicheza. Bila yeye nilianza kuyatatua matatizo yangu yote kwa kunywa pombe. Nilikuwa nakunywa pombe nyingi kupita kiasi na sikuweza kutembea,” ndivyo anavyoanza kusimulia straika aliyetarajiwa kuitikisa dunia lakini hajafika popote kisoka na tangu baba yake afariki dunia, amepotea kwenye ramani.
Mbrazili huyu, Adriano, 35, alitarajiwa atakuwa mmoja wa wachezaji bora wa dunia lakini simulizi yake imeishia njiani na kikubwa kinachotajwa kama sababu ni baada ya kufariki dunia kwa baba yake mzazi. Adriano ambaye nchini Italia alifahamika kama L’Imperator (The Emperor au Mtawala), tangu mwaka jana anaichezea Miami United! Utakumbuka kwamba Adriano aliiteka dunia na kuwa gumzo kubwa tangu alipoonyesha kiwango cha hali ya juu kwenye michuano ya Copa America 2004.

Hata hivyo, alijulikana miaka mitatu kabla akiwa ni kinda mwenye miaka 19 katika kikosi cha Inter Milan. Kila aliyemshuhudia alikiri kuwa huyu atakuwa mmoja wa mastaa wakubwa mno duniani. Mbrazili huyu alijitambulisha duniani kwa bao kali la faulo alilofunga dakika ya mwisho walipoifunga Real Madrid 2-1 kwenye mechi ya kirafiki.
Akiwa kinda, alianza kupata nafasi kufuatia majeraha ya Ronaldo de Lima ambaye alipata majeraha yaliyomweka nje ya uwanja kwa muda mrefu. Kurejea kwa gwiji huyo aliyeshinda mataji mawili ya Mchezaji Bora wa Dunia (Ballon d’Or) yalisababisha Adriano apelekwe kwa mkopo katika kikosi cha Fiorentina katikati ya msimu wa 2001-02 — baadaye Inter ikaingia katika makubaliano ya kubadilishana na Parma ili imnase Fabio Cannavaro.
Mbrazili huyo akaenda Parma ambako alitengeneza kombinesheni matata na Adrian Mutu mpaka pale Mutu alipotimkia Chelsea. Mwaka 2004, Brazil walikwenda katika michuano ya Copa America wakiwa wanapewa nafasi kubwa ya ubingwa na Adriano ndiye aliyekuwa supastaa wao.
Na hakuwaangusha. Nyota huyo aliyekuwa na umri wa miaka 22, aling’aa kwenye michuano hiyo nchini Peru. Mabao yake saba yalimpa Kiatu cha Dhahabu huku uhodari wake kwenye fainali ukiipa Brazil kombe lake la saba la michuano hiyo.
Argentina ilionekana inakwenda kumaliza ukame wa miaka 11 wakati Cesar Delgado alipowawezesha kuongoza 2-1 zikiwa z i m e baki dakika tatu kabla ya mpira kumalizika. Lakini Adriano akasawazisha ndani ya dakika tatu za nyongeza na akafunga penalti ya kwanza wakati Brazil walipowatoa nishai wapinzani wao hao kwa changamoto ya mikwaju.
Tangu hapo alikuwa ameshaiteka dunia na klabu yake ya zamani, Inter, ikaamua kumnunua tena. Hata hivyo, janga kubwa lilitokea mwishoni mwa 2004 baada ya dunia ya Adriano kugeuka juu chini kufuatia kifo cha baba yake mzazi, Almir, ambaye alifariki dunia kwa shambulio la moyo.
Kabla ya kifo hicho, Adriano alikuwa gumzo kubwa na alikiri kwamba motisha yake kubwa zaidi uwanjani ilikuwa ni kumuona baba yake akiwa na furaha baada ya kumpa sapoti kubwa mno wakati anakua. Adriano hakuweza kukabiliana na msiba huo na akaanza kunywa pombe kupita kiasi. Kuna wakati hakwenda mazoezini baada ya pombe za usiku alipokesha klabu kumzidia.
Hayo ndiyo yakawa maisha mapya ya Adriano. Mara mbili alikamatwa akijirusha kwenye klabu za usiku za Milan msimu wa 2006-07 wakati kesho yake timu yake ikiwa na mchezo muhimu, hali hiyo ilimlazimu rais wa klabu, Massimo Moratti amrudishe Brazil kwa likizo isiyo na malipo. Adriano alifurahia maisha kidogo mno wakati Jose Mourinho alipochukua mikoba ya kuinoa Inter.
Lakini kabla msimu haujaisha, Inter iliona haiwezi kuendelea naye na straika huyo akarudi Flamengo mwaka 2009. Adriano aling’aa Brazil na kuisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wake wa kwanza tangu 1992 huku yeye akifunga hat trick (mabao matatu) mbili.
Haraka, baada ya kuona hivyo, AS Roma ikaamua kumchukua staa huyo aliyekuwa na miaka 28 kwa mkataba wa miaka mitatu lakini ikauvunja baada ya miezi saba tu kufuatia kukosa ilichokitarajia. Mwaka 2011, Adriano ambaye alikuwa akionekana mwenye umri mkubwa na kiasi fulani cha kitambi, akajiunga na Corinthians na kutwaa ubingwa mwingine wa ligi ya Brazil.
Lakini aliachwa mwaka mmoja tu baadaye kutokana na ulevi. Januari 2016, baada ya miaka minne ya kutokuwa na shughuli uwanjani, alisaini mkataba na Miami United. Hilo ndilo jaribio lake la mwisho, hata hivyo inaonekana wakati wake wa kuwa levo za juu, umetoweka hata kabla haujatokea. Huyu ndiye Adriano, unaweza kuona jinsi kifo cha baba yake kilivyomharibia maisha!