MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu, leo ameongoza maadhimisho yanayoitwa Siku ya Mto Nile yaliyofanyika jijini Dar es Salaam yakitanguliwa na matembezi yaliyoanzia viwanja vya Mnazi Mmoja na shughuli nyingine zilizokuwa zikifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Maadhimisho hayo ni ya nchi wanachama wa Umoja wa Ushirikiano wa Mto Nile (NBI) ambapo zinaadhimisha mwaka wa 18 tangu kuanzishwa umoja huo mwaka 1999.

Makamu wa Rais, Bi Samia Suluhu (kulia) akizungumza wakati wa maadhimisho hayo
Maadhimisho hayo yanalenga kukuza uelewa kwa watu wote kuhusu umuhimu wa ushirikiano baina ya nchi zote 10 wanachama juu ya masuala yanayotekelezwa na faida inayopatikana kutokana na matumizi bora ya rasilimali za bonde la mto huo.
Miongoni mwa nchi 10 wanachama wa NBI ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Sudan, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Misri. Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka Februari 22 katika nchi mojawapo mwanachama.
NA DENIS MTIMA/GPL