×

Liuzio: Yanga Wakijipindua Kidogo tu, Wameisha Aisee

Wilbert Molandi | CHAMPIONI JUMAMOSI| Dar es Salaam

STRAIKA wa Simba aliyekuwa anakipiga Zesco ya Zambia, Juma Liuzio ametamba kuwa kamwe hawaiogopi Yanga, bali wanaiheshimu ila wakiwadharau basi watashinda leo. Liuzio, mwenye bao moja tu katika Ligi Kuu Bara, leo Jumamosi anatarajiwa kuwemo katika kikosi cha Simba kitakachoivaa Yanga kwenye mchezo wa marudiano wa ligi hiyo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Liuzio alisema siku zote hakuna timu nyepesi, zote ngumu, kikubwa kinachotakiwa ni kujiamini pekee ndani ya uwanja na mpinzani wako akikudharau unaweza kumfunga.

Liuzio alisema, hii ni mechi yake ya kwanza kucheza itakayowakutanisha Simba na Yanga katika ligi, hivyo amejiandaa vizuri kuhakikisha wanashinda mchezo huo.

“Mimi hii ni mechi yangu ya kwanza ya Simba na Yanga, kiukweli siyo mechi nyepesi, ni ngumu kutokana na kuzikutanisha timu zenye mashabiki wengi.

“Hivyo, mimi binafsi nimejiandaa kwa ajili ya mechi hiyo ambayo ni ngumu, niseme tu siwaogopi Yanga, lakini ninawaheshimu tu kwani ni timu nzuri yenye ushindani,” alisema Liuzio.

“Tatizo ni moja tu, Yanga wakitudharau tu ni lazima tuwafunge maana huu ni mchezo muhimu kwetu sote.”