
Siku moja baada ya mwanadada mwenye mvuto wa kipekee kutoka kwenye kiwanda cha Bongo Movie, Wema Sepetu kutangaza kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), msanii wa vichekesho na filamu za Kibongo, Steven Mengere (Steve Nyerere), ameibuka na kufunguka mambo mazito kuhusu msanii huyo na mama yake mzazi, Miriam Sepetu ambaye naye amehamia Chadema.


Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye Ukumbi wa Millenium Tower, Makumbusho jijini Dar es Salaam, Steve Nyerere alimlaumu mama Wema kwa kitendo chake cha kuvujisha mazungumzo ya sauti, aliyoyafanya kati yake na mwanamke huyo, kisha kuyavujisha kwenye mitandao ya kijamii.


Nyerere alisema kitendo hicho kimemhuzunisha sana na haelewi kwa nini mama Wema alifikia hatua hiyo wakati kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiishi vizuri pamoja, akaongeza kwamba kama kuna kosa amewahi kumfanyia, anaomba amsamehe.


Kwa upande wa Wema, Steve Nyerere alisema kwamba madai aliyoyatoa msanii huyo kwamba ametapeliwa na CCM fedha zake za kampeni, hayana ukweli wowote kwa sababu, yeye (Steve) ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kampeni kwa upande wa wasanii, wakimnadi mama Samia Suluhu Hassan kupitia kampeni ya Mama Ongea na Mwanao na kwamba fedha zote walilipwa wakiwa jijini Mwanza.

Steve Nyerere akahitimisha kwamba yeye amekuwa kada wa CCM kwa muda mrefu na kamwe hawezi kukihama chama hicho, hata kama Wema amehamia Chadema.
Tazama video…