
Wilbert Molandi | CHAMPIONI| Dar es Salaam
KOCHA Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi amesema matokeo ya timu yake kufungwa mabao 2-1 na Simba yanaendelea kuwavuruga wachezaji wake licha ya kuwa zimeshapita siku kadhaa tangu kuchezwa kwa mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara.
Mwambusi aliitoa kauli hiyo mara baada ya kumalizika kwa mechi ya ligi kuu kati ya Yanga na Ruvu Shooting, juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar ambapo timu yake ilishinda kwa mabao 2-0.
Katika mechi dhidi ya Simba, mabao ya washindi yalifungwa na Laudit Mavugo na Shiza Kichuya huku lile la Yanga likifungwa na Simon Msuva kwa njia ya penalti. “Kama unavyojua timu inapotoka kupoteza mchezo wa nyuma ambao ni muhimu kwetu ambao kama tungeshinda, basi tungekaa kileleni kidogo morali ya wachezaji na saikolojia yao inapungua.
“Sisi Yanga tulipoteza mechi iliyopita na Simba kiukweli matokeo yalituchanganya, ni mechi muhimu tuliyohitaji ushindi wowote ili tukae kileleni na tuendelee kuutetea ubingwa wetu, lakini matokeo yakawa tofauti.
“Lakini nimefurahi mechi hii ya Ruvu vijana wangu walijitahidi kucheza kwa kujituma tukiwa pungufu na kufanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-1, hivyo bado hatujakata tamaa, tutapambana hadi mwisho wa ligi ili tuchukue ubingwa,” alisema Mwambusi.