
MEYA wa Wilaya ya Kinondoni na Diwani wa Kata ya Msasani jijini Dar es Salaam, Benjamini Sitta amezindua michuano ya soka itakayojumuisha kata 16 zilizopo katika Kata ya Msasani.

Mashindano hayo yaliyopewa jina la Sitta Cup 2017, yamezinduliwa jana ambapo meya huyo amegawa mipira kwa timu zote shiriki.
Akizungumza na wanahabari wakati wa uzinduzi huo, Sitta alisema kuwa mashindano hayo yatakuwa yakifanyika kwenye Uwanja wa Magunia maarufu kama Bonde la Mpunga Msasani.

Alieleza kuwa lengo la mashindano hayo ni kuwaweka karibu vijana ili waweze kuwa jamii moja kupitia soka, kujenga undugu na uraia na pia kuondokana na matumizi ya madawa ya kulevya.

“Mashindano haya yanaratibiwa na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na ni moja ya utekelezaji wa ilani ya CCM, tunataka kufufua vipaji vya vijana na nawashukuru waratibu na watu wengine ambao wamefanikisha zoezi hili.

“Bingwa wa michuano hii atazawadiwa Sh milioni mbili, mshindi wa pili Sh milioni moja, mchezaji bora atapewa Sh milioni moja, kiungo bora naye atapewa zawadi na hata washangiliaji nao watapata zawadi,” alisema Sitta.










Aidha alisema kuwa mbali na zawadi za fedha, pia kutakuwa na zawadi za pikipiki ambazo zitatolewa kwa washindi mbalimbali.
Naye mratibu wa mashindano hayo, James Mwakibinga, alisema kuwa anayaomba makampuni na wadau mbalimbali kuunga mkono michuano hiyo ili kuiwezesha kufanikisha lengo la mstahiki meya ya kuimarisha michezo ndani ya Kata ya Msasani.
NA DENIS MTIMA/GPL