
Mwanasiasa, mwanaharakati na mpigania uhuru mahiri nchini Tanzania, Sir George Kahama (88), amefariki dunia leo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Kwa mujibu wa Kaimu Afisa Habari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, John Steven, Kahama amefariki leo majira ya saa 10 jioni, huku maradhi yaliyosababisha kifo chake yakiwa bado hayajawekwa wazi.
Enzi za uhai wake, Kahama amewahi kuwa Waziri wa mambo ya Ndani wa Tanganyika (1961- 1962) na alikuwa msaidizi wa karibu wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mara ya mwisho, Kahama alionekana kwenye majukwaa ya kisiasa akiwa na aliyekuwa akiwania kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM, Benard Membe.