×

Serengeti Boys Wapewa Kadi za Bima ya Afya

Na Ibrahim Mussa/CHAMPION/GPL

WACHEZAJI wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, jana walikabidhiwa Kadi za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Shirika la Bima la Afya la Taifa (NHIF) kwa lengo la kuwasaidia kupata matibabu ya uhakika wanapokuwa wanaumwa.

Timu hiyo kwa sasa inajiandaa na michuano ya mataifa Afrika kwa vijana inayotarajiwa kufanyika nchini Gabon, Mei, mwaka huu.

Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa NHIF, Angela Mziray, amesema kuwa lengo la kutoa kadi hizo kwa wachezaji hao ni kuwasaidia kupata matibabu kwa urahisi katika vituo vyote nchini hata wakiwa nje ya majukumu ya timu ya taifa.

“Kadi za Bima ya Afya zinatoa mfumo rahisi wa kuweza kupata matibabu na lengo la kufanya hivi ni kuweza kuwasaidia vijana hawa ambao ni matarajio ya kesho kwani hii siyo mara ya kwanza kufanya kazi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na sasa hivi tunatoa huduma katika vituo 6,500 nchini.

Kiukweli hili siyo jambo dogo kwa vijana wetu, maana linaleta hamasa na umuhimu mkubwa kutokana na wao kuweza kuwa na uhakika wa kupata huduma bora za afya kwa kadi ambazo tunawapatia kwa sababu wao wanafanya mazoezi na wanaweza wakaumia, hivyo zitawasaidia katika kupata huduma nzuri bila ya kutumia pesa yoyote kutoka mkononi mwao,” alisema Mziray. Upande wa Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, alisema wanaushukuru mfuko huo kutokana na mchango huo walioutoa kwa timu hiyo huku akiwaomba wawe sehemu ya wadhamini wa timu hiyo inayojiandaa na fainali za Afrika nchini.