×

Hadithi ya Shigongo: Dimbwi la Damu-15

Baada ya Manjit kukabidhiwa 
kampuni yake na Multilat
eral Investiment Inc. kwa haraka alichukua uamuzi wa kuibadilisha  kampuni yake jina  na  kuiita Canada Oils & Gas Inc. Mabadiliko hayo yaliwafanya watu wengi kuamini  Manjit angeweza kuiendesha vizuri kampuni yake.

Alipangua ngazi zote za uongozi  kuanzia juu hadi chini na aliajiri Mkurugenzi mpya aliyemtoa katika kampuni ya Multilateral. Yeye alibaki kama mwenyekiti wa kampuni hiyo,  mama yake pamoja na Victoria wakawa wajumbe wa bodi.

Miaka mitatu  iliyofuata kampuni  yake ilishuhudia mafanikio makubwa  kupita kiasi,  vituo vya mafuta viliongezeka katika nchi nzima ya Canada! Canada oil & Gas Inc ilimiliki vituo vitatu hadi vinne vya mafuta katika kila miji mikuu yote nchini humo. Manjit akabadilika na mtu mashuhuri na kijana tajiri kuliko  hata alivyokuwa baba yake.

 “ Mama! Nitajitahidi kufanya kazi kwa nguvu zote  ili tufanikiwe zaidi!”

“Sawa mwanangu, kila utakachofanya ni sawa kwangu!”

Maneno ya mama yake yalimpa moyo sana Manjit, mwaka huo huo ilitangazwa tenda ya kuliuzia mafuta Dizeli na Petroli jeshi la nchi hiyo, ilikuwa ni  tenda ya mamilioni ya dola za kimarekani na ilikuwa ni kazi kubwa kuliko kazi zote alizowahi kufanya  tangu akabidhiwe kampuni.Wafanyabiashara wengi   nchini Canada waliitaka kazi hiyo na  kampuni ya Canada Oils& Gas nayo ilikuwa miongoni mwa kampuni zilizoiomba.

“Mama ni lazima tufanye  lolote  linalowezekana kuhakikisha tunapata tenda hii?”

“Fanya lolote mwanangu, kila kitu ni ruksa!”

“Ni lazima tutumie pesa mama! Sababu wanasema tumia pesa  ili upate pesa!”

“Sawa tu mwanangu!”

Hilo ndilo alilofanya Manjit,  alitumia pesa nyingi kuwahonga  watu wote waliokuwa na mamlaka ya kuitoa tenda  mpaka akaibuka mshindi! Ilikuwa ni furaha kubwa mno kwa Manjit, mama yake, Victoria na hata wafanyakazi wengine  wa kampuni hiyo!  Walijua kupatikana kwa kazi hiyo  kungeongeza maslahi yao.

“Mama   tumetajirika!”

“Hakika mwanangu! Nimeamini una akili”

“Itabidi nisafiri hadi Iran kwenda kuongea biashara na matajiri wa huko ikiwezekana tuwe tunapata mafuta ya mkopo kutoka kwao na kuwalipa baada ya  kupata malipo yetu kutoka serikalini!”

“Fanya uwezalo!”

Wiki moja  baada ya kupata tenda hiyo  ilibidi Manjit alisafiri hadi Iran ambako aliongea na wafanyabiashara wengi wenye visima vya mafuta lakini hakufanikiwa kupata hata mmoja aliyekuwa tayari kufanya naye biashara, kila aliyemfuata  na kumweleza kuwa mahitaji yake ya mafuta yalikuwa mapipa milioni mbili kwa mwezi, aliiona kazi hiyo ni kubwa sana na kukiri asingeweza kukidhi haja yake!

“Nafikiri ungejaribu  Iraq  kuna kampuni moja inaitwa Gulf Gas Limited hiyo inaweza kukupa mafuta hata zaidi ya hayo!”

“Inamilikiwa na nani?”

“Awali ilimilikiwa na Mohamed Mashreef huyo alikuwa mfanyabiashara  wa Kiarabu lakini alifariki na kumrithisha Mwafrika mmoja, ninavyosikia yeye pia ni mgonjwa   kazi zote hivi sasa zinaendeshwa na mtoto wake aitwaye Patrick!”

“Patrick?”

“Ndiyo!”

“Mbona jina si la kiarabu?”

“Ni mchanganyiko wa Mwarabu na Mtanzania!”

“Mtanzania?”

“Ndiyo, baba yake alitokea Tanzania miaka mingi iliyopita!”

“Nahitaji kumwona!”

“Basi safiri mpaka Iraq!”

Siku hiyo hiyo jioni Manjit alipanda ndege na kusafiri  hadi Baghadad ambako aliingia usiku na kushindwa kumtafuta tajiri Patrick  ikabidi alale mpaka siku iliyofuata asubuhi alipokwenda ofisini kwake! Nje ya ofisi hiyo kulikuwa na idadi kubwa sana ya  maaskari walionekana kuimarisha ulinzi lakini  Manjit alifanikiwa kuingia hadi mapokezi  baada ya kujitambulisha,  mapokezi alipokelewa  na  msichana mrembo wa Kiarabu na kukaribishwa  aketi kitini!

“Can I see the Director?”

“Sorry the Director is not around! He is admitted in hospital, but his Deputy is around, would you like to see him?” (Mkurugenzi hayupo lakini  Naibu wake yupo, je ungependa kumwona yeye?)

“Yeah! Because this is an official matter I think it can be be handled by any authority! (Ndiyo kwa sababu hili ni suala la kikazi  na  linaweza kushughulikiwa na mtu yeyote!)

Baada ya jibu hilo msichana  huyo alinyanyua simu yake na kubonyeza namba fulani  kisha akaanza kuongea na mtu wa upande wa pili  na  kumueleza kuwa palikuwa na mgeni aliyetaka kumuona!  Alipoweka simu yake chini alimuashiria Manjit aingie ndani! Alinyanyuka na kuanza kutembea  taratibu akiufuata mlango uliokuwa kulia kwake ilikuwa ni   ofisi  ya kifahari, iliyopambwa na vioo kila upande! Iliashiria kuwa  mwenye ofisi hiyo alikuwa na uwezo mkubwa kipesa! Manjit aliingia  ndani akiwa na hamu  kubwa ya kumuona Patrick, mawazoni kwake alifikiri mtu huyo alikuwa  anakwenda kumwona  ni  mnene na mzee lakini alishangaa kukuta mtu aliyekuwa akimtafuta ni kijana mdogo kuliko hata yeye!

“You are welcome sir!”(Karibu sana bwana!)

“Thank you! I’m Mr. Manjit Shabir!”(Ahsante! Ninaitwa Bwana Manjit Shabir)

“Manjit Shabir? The owner of the Oil company in Canada!”(Manjit Shabir? Mwenye kampuni ya Mafuta Canada?)

“Oh yeah!How did you recognise me?”(Ndiyo umenigunduaje?)

“Nice to meet you Sir, I’m Patrick N. Abdulwakil I have been hearing of your name so many times and really wanted to meet you one day! Today my dream has come true!”(Nimefurahi kukutana na wewe! Ninaitwa Patrick N. Abdulwakil nimekuwa nikisikia jina lako mara nyingi na nilitaka sana kukutana na wewe siku moja! Leo ndoto yangu imetimia!) Alisema Patrick akinyanyuka na kumkumbatia Manjit, walionyesha furaha kubwa sana.

Waliongea mambo mengi kuhusu biashara yao ya mafuta na  hatimaye kufikia muafaka wa kufanya biashara kwa ushirikiano! Patrick alikubali kumuuzia Manjit mafuta kwa mkopo  kwake kazi yake pekee ingekuwa ni kuyasafirisha mafuta kutoka Baghdad kwenda Montreal Canada na angetakiwa kulipa pesa baada ya kuyauza mafuta kwa jeshi! Kwa Manjit mambo yalikuwa kama alivyopanga, hakutegemea mipango ingekuwa rahisi kiasi kile furaha yake ilizidi kuongezeka.

“Lakini kumbuka kuwa kampuni  yangu haitawajibika na hasara yoyote itakayotokea katika usafirishaji wa mafuta, hata kama meli itazama sisi  tutakachojua ni  kulipwa pesa yetu tu, sijui jambo hilo utaliweza?”

“Haina shida kabisa Patrick! Hilo litafanyika!” Alijibu Manjit  na mkataba ulisainiwa  siku hiyo hiyo Manjit aliondoka  kurudi Canada bila kuelewa undugu na uhusiano uliokuwepo kati yao.

***************

Kwa Manjit kupata tenda ya kuliuzia jeshi mafuta  ilikuwa furaha kubwa na dalili ya mafanikio lakini  kwa wafanyabiashara wenzake walioikosa  tenda hiyo  hasira ziliwajaa, hasira zilizojaa chuki  dhidi ya Manjit hasa baada ya kugundua kuwa Manjit alitumia pesa kuwahonga  viongozi wa jeshi ndio akapata tenda hiyo, walichukia mno na kulazimika kuunda umoja wa kupambana naye, waliahidi kumkwamisha katika biashara zake zote!

“Ni  lazima aanze moja, naona hizi mali za kurithi zimempa kiburi anashindwa kuheshimu wazee, huyu ni mtoto mdogo sana hawezi kutusumbua sisi!” Alisema bwana Davids, mmiliki wa kampuni ya kusafisha mafuta machafu nchini Canada, Crude Oils Inc.

“Kweli! Ni lazima tumkomeshe” Wenzake watano waliitikia.

Mipango mingi ilipangwa usiku huo ili kumwangusha Manjit kibiashara, matajiri waliokosa tenda ya kuuza mafuta jeshini waliunganish nguvu zao ili  kupambana nae! Miongoni mwa mipango yaliyopanga ni kumuua Manjit mwenyewe na kama si yeye basi mama yake au Victoria!  Ili mradi tu kuhakikisha anarudi  nyuma na kufilisika  kabisa! Hawakuwa tayari hata kidogo kuona mtoto mdogo tena mgeni  katika nchi yao akitajirika mbele ya macho yao!

“Nitazilipua meli zote za mafuta zitakazokuwa zikibeba mafuta yake kutoka Iraq kuja hapa Canada! Hilo niachieni mimi” Alisema Alexandria   mmiliki wa vituo vya mafuta vya CanadOils

“Nitatuma watu kuivamia nyumba yake  na kila mtu atakayekuwemo ndani  siku hiyo ni lazima afe hata yeye mwenyewe!” mfanyabiashara mwingine aliahidi.

“Nitatumia watu wa  Mamlaka ya kodi ili wayakague mahesabu yake  kuona kama analipa kodi, nina uhakika atakuwa na matatizo makubwa! Na hapo ndipo tutakapomaliza! Canadian Revenue Authority watakamata mali zake zote!” Mwingine tena aliongea kwa hasira!

Yote yaliyosemwa  katika mkutano huo hayakua utani, wazee hao walidhamiria kumkomesha Manjit! Walidhamiria kumfanya masikini na hata kumuua kabisa yeye na familia yake yote. Manjit hakujua lolote lililoendelea mioyoni mwa wafanyabiashara wenzake na aliamini hakuna aliyeijua siri yake ya kushinda zabuni hiyo ya kuuza mafuta.

********************

Meli tatu za kwanza zilizobeba matenki ya mafuta ya karibu dola milioni 120 ambazo kwa wakati huo zilikuwa sawa na shilingi za Kitanzania Bilioni 84  zilikuwa zikisafiri katika bahari ya  Hindi kuelekea Canada, pamoja na kubeba mafuta ndani ya meli hizo kulikuwa na wafanyakazi wasiopungua mia mbili na kumi!

Huo ndio ulikuwa mzigo wa kwanza ambao Manjit alitegemea kuumwaga jeshini  Canada na kupata faida ya dola za Kimarekani zisizopungua 200! Ilikuwa ni faida kubwa mno iliyompa uhakika  asilimia mia moja kuwa kama angefanya biashara hiyo kwa mwaka mmoja angeweza kutajirika  pengine kuliko mtu mwingine yeyote katika nchi hiyo.

Alikuwa nyumbani kwake akipumzika na familia yake  ikiwa ni siku mbili tu  tangu aongee na tajiri Patrick  akipewa taarifa kuwa  tayari mzigo ulishaondoka nchini Iraq na ulitegemewa kuingia Canada baada ya wiki tatu! Ghafla simu yake iliita na  mama yake aliipokea na kumpa Manjit.

“Hallow! Manjit  anaongea nani mwenzangu?”

“Mimi ni Patrick!”

“Ndiyo za tangu juzi?”

“Ni nzuri lakini sio nzuri sana!”

“Unaumwa?”

“Hapana ila nina taarifa mbaya kidogo, meli zote zilizoondoka hapa   na mafuta    zimelipuliwa! Wafanyakazi  wote wamekufa na meli bado zinawaka moto huku matuta   yakimwagika baharini, nilipoteza nao mawasiliano tangu jana leo nimepokea simu ya upepo kutoka kwenye meli ya Atlantic Sailors, wamenitaarifu kuwa waliiona meli yetu ikiwaka moto baharini! ”

“Mungu wangu unaniambia kweli?”

“Huo ni ukweli siwezi kukudanganya hata mimi nimechanganyikiwa! Nafikiri  kwako itakuwa  hasara kubwa sana, kwa  kweli biashara umeianza vibaya kwani  sisi mafuta yetu itabidi yalipwe kama kawaida!”

Taarifa hiyo ilimfanya Manjit alie machozi  kwani zilikuwa ni habari mbaya mno kwake, alijua ni njama lakini alishindwa kuelewa ni nani aliyezifanya  hata mama yake pamoja na Victoria  nao walishindwa kuvumilia  wakajikuta wakibubujikwa na machozi!

Siku iliyofuata ilibidi  Manjit asafiri hadi Iraq  kuongea na Patrick ambaye aliendelea kusisitiza juu ya makubaliano yao katika mkataba ulioeleza wazi kuwa  Manjit alitakiwa kulipa pesa zote alizodaiwa pamoja  na kuwa mafuta yalimwagika baharini! Manjit hakuwa na ubishi alikubali kufanya hivyo lakini si kwa wakati huo.

Patrick alikubali na kumpakilia tena meli nyingine nne zenye mafuta ya thamani ya dola milioni 600 ambazo kwa  shilingi  za Kitanzania zilikuwa ni sawa na bilioni 480  kwa wakati huo, lakini pia meli hizo    hazikufanikiwa kufika  nchini Canada, zikiwa katika eneo lile lile zilipolipukia meli za mwanzo nazo ziliangushiwa mabomu na kulipuka! Mafuta yote yalimwagika na watu wote waliokuwemo  waliteketea kwa moto, Manjit alizidi kuchanganyikiwa na kushindwa kuelewa ni nani aliyekuwa akimfanyia ukatili huo!

Alipoongea na Patrick juu ya tatizo hilo yeye aliendela kusisitiza juu ya malipo yake!  Tayari deni lilishafika dola za Kimarekani milioni 720 Zilikuwa ni pesa nyingi  mno kwake kuzilipa na kuendelea kufanya biashara, pamoja na matatizo yote hayo Manjit hakukata tamaa alijipa matumaini kuwa angeweza kulipa deni hilo baada ya kufanya biashara na jeshi kwa muda, hivyo aliomba apakiliwe mafuta mengine  tena na Patrick alikubali.

Kwa hasira ya kufidia safari hii alipakia  katika meli saba zote zikiwa na mafuta ya thamani dola   milioni 800, ilikuwachenga waliokuwa wakimhujumu nne  kati ya meli hizo zikapita njia ya kawaida  na tatu zikapitishwa njia ya mzunguko  wa CapeTown, Afrika Kusini kisha  kwenda Afrika ya Magharibi  na baadaye  kuingia Canada, kwa njia hiyo Manjit aliamini angeweza kufikisha mafuta yake hata kidogo.

Meli zote saba hazikufanikiwa kufika Canada, zote  zililipuliwa zikiwa njiani! Manjit alichanganyikiwa zaidi, deni alilokuwa nalo kwa Patrick lilimtisha! Aliamini tayari alishakuwa masikini  na angeweza hata kufungwa gerezani kama angeshindwa kulipa pesa za Patrick.

Kwa hakika maadui zake tayari walishafanikiwa kumporomosha. Akilia machozi aliamua kurudi nyumbani kutafuta pesa za kumlipa Patrick.

*******************

Aliteremka uwanja wa ndege wa Ottawa saa kumi na mbili jioni na kuchukua teksi.

“Nipeleke Carvin Avenue!”

“Sawa mzee!”

Gari liliondoka uwanja wa ndege kwa kasi  na kadri  lilivyozidi kuyakaribia   maeneo ya nyumbani kwake   Manjit alizidi kusikia kelele za ving’ora vya magari ya zimamoto!  Awali alifikiri yalikuwa ni mambo ya kawaida  katika jiji hilo lenye watu   na pilikapilika nyingi za maisha, lakini  hatua chache kabla ya kufika nyumbani kwake alishangaa kuona moshi mkubwa angani, alipoingalia nyumba yake hakuiona ilikuwa katikati ya moshi.  Moto mkubwa ulikuwa ukiiteketeza, zimamoto walikuwa wakijitahidi kuzima lakini walishindwa.

Hakufikiria kitu kingine chochote, mawazo yake  yalimpeleka kwa mama yake mzazi pamoja na Victoria aliowaacha ndani ya nyumba yake!  Kwa haraka aliruka garini na kuanza kukimbia  mbio kuelekea kwenye moto huo mkubwa  huku akiliita jina la mama yake!  Aliona ni heri kufa kuliko kupambana na matatizo yaliyokuwa yakimfuata, mbele kidogo alisita na kusimama, woga wa kuungua na moto ulimwingia.

Kwa hakika dunia ilikuwa imemgeuka! Deni la mafuta  alilokuwa akidaiwa hakuwa na uwezo wa kulilipa na bado nyumba yake ilikuwa ikiwaka moto na hakuwa na uhakika kama mama yake pamoja na Victoria walikuwa hai au walikuwa wakiteketea ndani ya moto huo.

Kwa jinsi umati mkubwa wa watu ulivyokusanyika hakuna mtu aliyegundua kuwa Manjit alikuwepo eneo la tukio,  akiwa amesimama   wima huku akitetemeka   alisikia sauti ya mama yake ikiliita jina lake kutoka katikati ya moshi mkubwa uliotanda eneo hilo, hiyo ilimaanisha mama yake alikuwa bado amekwama ndani ya nyumba iliyokuwa ikiwaka moto!

Moyo wake ulimuuma  kupita kiasi na kujikuta akipata  ushujaa wa ajabu na kuanza kukimbia mbio kuelekea ndani ya nyumba iliyokuwa ikiwaka moto bila woga kama ilivyokuwa awali.

Manjit alijua yaliyotokea yote yalikuwa ni  hujuma lakini hakujua ni nani aliyemfanyia hujuma hiyo mbaya.

Watu waliokuwa eneo hilo walimwona mtu akikimbia kuingia ndani ya moto, kitendo hicho kiliwashangaza sana na kujikuta wakijaribu kukimbia kwa nyuma wakimfuata kwa lengo la kumuokoa lakini tayari Manjit alishapotelea  ndani ya moshi mkubwa uliokuwa umetanda! Walijua naye anakwenda kuteketea.

“Huyu sijui mjinga? Sasa kwanini ameingia ndani ya nyumba inayowaka moto kiasi hiki?” Walijiuliza baada ya kushindwa kumpata.

 ***

Masaa mawili kabla 
nyumba ya Manjit 
kulipuliwa  kwa moto na majambazi waliotumwa na wafanyabiashara maadui zake, Leah  na Victoria  waliondoka kwenda kula chakula  cha usiku katika mgahawa wa Foodmasters uliokuwa hatua  chache tu kutoka nyumbani kwao, cha kushangaza siku hiyo wote wawili hawakutaka kula chakula cha kupikwa nyumbani. Kokote alikokwenda nje ya nyumba Victoria hakukisahau kipande cha noti walichogawana na kaka yake, alikuwa tayari kupoteza vitu vingine vyote lakini si kipande hicho

Ghafla wakiwa katika mgahawa huo kabla hata chakula hakijaletwa walishutshwa na mlio ya ving’ora vya magari ya zima moto vikipita kwa kasi kubwa nje ya mgahawa.

Kila mtu alionyesha mshangao mkubwa na kilichofuata baada ya ving’ora hivyo  ulikuwa ni moshi mkubwa ulioonekana kuzunguka maeneo ya nyumba yao, Leah alishtuka sana na kukimbia kwenda nje ya mgahawa akiwa amemshika   Victoria mkono, nje alimwigiza ndani ya gari na safari ya kurudi nyumbani kwao ilianza haraka!

“Dada kuna nini?”

“Moto, moto unawaka?Sijui ni nyumbani kwetu?”

“Moto? Nyumbani kwetu?”

“Ndiyo!”

“Haiwezekani dada!” Kuna wakati Victoria alimwita Leah mama na wakati mwingine alimwita dada, alishindwa atumie jina gani.

“Acha twende tukaangalie!”Alisema Leah akiliendesha gari lake kwa kasi kubwa, mapigo ya moyo   yalikuwa yakienda kwa kasi kubwa,  walivyozidi kukaribia dalili zote zilionyesha kuwa ni nyumba yao iliyokuwa ikiungua! Kadri alivyozidi kuelekea nyumbani ndivyo moto na moshi ulivyozidi kuongezeka.

“Ni nyumba yetu!” Leah alisema akimpigapiga Victoria begani.

“Imeungua?”

“Ndiyo  inaungua na sijui nini kimetokea mpaka   ikashika moto! Kwanini matatizo yamekuwa mengi kiasi hiki kwetu?” Alijiuliza Leah bila kujua la kufanya.

Bila kutegemea machozi yalianza kumtoka kwani  vitu vingi vyenye thamani   vilikuwa vimeungulia ndani ya nyumba  yao, roho ilimuuma sana Leah. Kwa matatizo waliyokuwa nayo katika familia yao alijua tayari walikuwa wamekwisharejea katika umasikini! Leah alikata tamaa!

“Tutafanya nini sisi? Manjit nae ana madeni ya mamilioni ya dola za watu, tutakuwa wageni wa nani sasa?” Alijiuliza Leah huku akilia! Muda wote   akiwa  amekumbatiana na Victoria wote wakilia.

Ghafla bila kutegemea jambo hilo Victoria alishtukia Leah akichomoka kutoka mikononi mwake na kuanza kukimbia   kwenda mbele , kwa jinsi hali  ya joto  ilivyokuwa  mahali waliposimama  pamoja na kutokuona Victoria alijua  lazima Leah alikimbilia motoni!

Victoria alianza kulia akipiga kelele na kuomba msaada huku nae akijaribu kutembea taratibu kwenda mbele    akiita  jina Leah kwa sauti ya juu.

“Dada Leah! Dada Leah! Dada Leah! Uko wapi?” Alisema huku akizidi kutembea kwenda mbele zaidi.

Hakusikia sauti ya Leah ikiitika mahali popote na joto lilizidi kuongezeka, moto  nao ulizidi kuwaka kuelekea mahali aliposimama, mara ghafla alishtukia akinyakuliwa na mikono mikubwa na mazito ya mwanaume!

“Wewe unafanya nini hapa wakati moto unakuelekea? Utawaka ohooo!”

“Dada yangu ameingia ndani ya moto,  dada yangu ameingia ndani ya moto! Tafadhali mtoeni!”Alizidi kulia.

“Ameingiaje?”

“Amekimbilia ndani tu!”

“Kwanini?”

“ Hii ni nyumba yetu!”Alizidi kueleza Victoria huku akilia.

Ilikuwa ni mikono ya  mtu wa  zimamoto  alimchukua victoria na kwenda kumkalisha  mbali kabisa ya moto! Ambako Victoria alikaa na  kuendelea kulia akijua wazi Leah alikuwa amejiua motoni,  alikuwa ameamua kuteketea pamoja na nyumba na vitu vyao.

Nusu saa  baadaye watu wengi walifurika eneo la tukio  wakishangaa na miongoni mwao alikuwepo Manjit aliyekuwa amerejea  nchini Canada kutoka Baghdad muda mfupi kabla!

******************

Manjit aliumia sana moyoni mwake kuona nyumba yao ikiteketea, aliamini mama yake pamoja na Victoria walikuwa ndani ya moto huo! Bila hata kusita aliamua  kukimbia kuelekea ndani ya jengo  kwa lengo la kwenda kuwaokoa Victoria na mama yake Leah!    Mbele kidogo moshi mkali ulijitokeza  akawa haoni mbele yake, akashindwa kusonga mbele   na   kugeuza  akikimbia kurudi nje! Alifanikiwa kutoka hadi nje ya jengo ambako alifikia mikononi mwa maaskari wawili wa  Zima moto! Walimkatama na kumkimbiza hadi sehemu alipokalishwa Victoria na kuanza kumpepea kwa sababu alionekana kushindwa kuhema vizuri!

“Kifua chake kimejaa moshi hebu mpelekeni hospitali haraka!” Aliamuru mmoja wa maaskari na Manjit alinyanyuliwa haraka na kupakiwa ndani ya gari la  wagonjwa kukimbizwa hospitali  ambako aliwekewa mashine ya oksijeni   na dakika kama ishirini   hivi  baadaye alirejea katika hali yake ya kawaida na kuanza kulia akiomba aonyeshwe mahali mama yake  na Victoria walipokuwa!

“Mama yako bado hajaonekana ila Victoria yupo!”

“Mama yuko wapi? Naomba basi  mmlete hata  Victoria  niongee naye nina uhakika atakuwa anafahamu mahali mama alipo, mali si kitu kwangu ninachotaka ni mama yangu peke yake!” Alisema Manjit huku akizidi kulia, hakuugua mahali popote mwilini kwake.

Hali yake haikuwa mbaya hata  kidogo  na angeweza  hata kuruhusiwa kutoka wodini lakini madaktari hawakufanay hivyo baada ya kupewa taarifa kuwa alitaka kuingia ndani ya nyumba iliyowaka moto ili afe! Walizidi kumweka wodini hadi asubuhi ya siku  iliyofuata aliporuhusiwa na kupelekwa chini  ya uangalizi wa polisi hadi eneo la tukio na kushuhudia shughuli za uzimaji wa moto zikimalizika! Mtu wa kwanza kumwona mahali pale alikuwa ni Victoria, alimkimbilia na kukumbatiana kwa furaha.

“Anti Vicky mama yupo wapi?” Aliuliza baada tu ya kumbusu kila upande wa shavu lake!

“Alikimbilia kwenye moto! Hivyo atakuwa amekufa!”

“Hapana haiwezekani! Mama hawezi kufa”

“Ni kweli, mimi nilikuwa naye hadi mara ya mwisho, alichomoka mikononi mwangu na kukimbilia motoni, nina imani atakuwa amekufa!”Alisema Victoria akilia na wote walikumbatiana na kuendelea kulia, ilibidi waondolewe hadi hotelini ambako Manjit alipanga vyumba viwili na yeye na Victoria waliishi wakiangalia ni nini cha kufanya baada ya hapo! Kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwa Manjit na Victoria, Manjit alishindwa kuelewa ni nani aliyekuwa akimfanyia  hujuma hizo! Kilikuwa ni kitendawili alichoshindwa kabisa kukitegua.

Akiwa hotelini alizidi kumtafuta mama yake akiamini bado alikuwa hai, alitangaza hata katika  vyombo vingi vya  habari na kuahidi zawadi kubwa kwa mtu yeyote ile angefanikisha kupatikana kwa mama yake, lakini kwa masaa mengi   hakuna mtu hata mmoja aliyejitokeza kudai kumwona Leah! Manjit alizidi kuchanganyikiwa na hakujua kipi cha kufanya!

Siku ya tatu wakati watu wa idara ya Uokoaji wakiendelea na kazi  ya  uokoaji walikuta mabaki ya binadamu aliyeungua vibaya katika chumba kilichoonekana kuwa sebule, ingawa ilikuwa si rahisi kufahamu kama mabaki hayo yalikuwa ya mama yake   au la,  Manjit alilazimika kuamini hivyo na mazishi ya heshima zote yalifanyika, akaamini kuwa huo ndio ulikuwa mwisho wa mama yake! Akabaki na mtu mmoja tu aliyemtegemea nchini Canada, huyo hakuwa mwingine bali Victoria.

Ikiwa ni wiki moja baada ya mazishi  ya mama yake, vituo vyake vyote vya mafuta vilikamatwa na shirika la kodi nchini Canada, kwa madai ya kuchunguza kama Manjit alilipa kodi zake  sawa sawa, vituo vyote vilitiwa makufuli, wafanyakazi wote wakaondolewa na maaskari waliwekwa kuvilinda! Kifupi hali ilikuwa mbaya mno kwa Manjit! Kwani ni biashara hiyo peke yake aliyoitegemea katika maisha yake. Alishindwa kuelewa angeishije.

Mwezi mmoja baadaye alichukua pesa zake zote zilizokuwa benki na kulipa nusu ya deni la mafuta alilodaiwa na Patrick, akaunti yake ikabaki bila hata senti! Hakuelewa hata kidogo pesa za kumalizia deni  hilo angepata wapi,  Manjit alitamani kufa lakini alishindwa kuufikiria uamuzi huo  kwa sababu ya Victoria! Alishindwa kuelewa  angebaki na nani? Huo ndio ulikuwa wasiwasi  wake mkubwa,   kama Victoria  angekufa katika moto hata yeye  pia angefuata na wote watatu wangehamia kuzimu alikotangulia baba yake.

***************

Hali haikuwa nzuri pia nchini Iraq, Abdulwakil baba yake Patrick, alikasirishwa sana na kitendo cha mtoto wake kukopesha kiasi kikubwa cha mafuta bila kumshirikisha.

“Ulikuwa mgonjwa baba!”

“Pamoja na hayo yote lakini kwanini ulimkopesha mtu ambaye hana uwezo wa kulipa?”

“Baba, Manjit amekuwa mteja wetu wa muda mrefu na isitoshe alionyesha karatasi zake za zabuni ya kuuza mafuta jeshini! Niliona anafaa nikaamua kumpa mafuta”

“Haiwezekani ni lazima afikishwe mahakamani  ili ashinikizwe kulipa pesa hizo!”

“Sawa baba!”

Siku iliyofuata Patrick aliwaita wanasheria wa kampuni yao ofisini  na kuwapa  majukumu ya  kuhakikisha Manjit anakamatwa na kufikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo, ili kumshinikiza alipe deni alilodaiwa.

“Sawa mzee, tufanya kazi hiyo lakini ili iwe rahisi zaidi tafadhali muagizie aje hapa Iraq ili kuwa rahisi zaidi kumkamata!”

“Nitafanya hivyo leo na ninafikiri kesho atafika hapa!”

“Itakuwa vizuri sana!”

Jioni ya siku hiyo Patrick alipiga simu Canada na kumwomba Manjit apande ndege kwenda Baghdad  siku iliyofuata ili wapate kuliongelea deni lake na ni kwa jinsi gani angeweza kulilipa! Alimtahadharisha kuwa kushindwa   kwake kufika  Baghdad kungemaanisha kufikishwa mahakamani na kwa mujibu wa mikataba waliyowekeana  ni lazima angefungwa, Manjit hakuwa na la kufanya zaidi ya kukubali kwenda Iraq.

“Lakini nitasafiri na anti yangu ambaye ni kipofu, sitaweza kumwacha hapa Canada peke yake  watamuua!”

“Hiyo haina tatizo kabisa!”

Siku iliyofuata asubuhi Manjit na Victoria walipanda ndege ya shirika la ndege la Gufl kwenda Baghdad, ndani ya moyo wake Victoria ilikuwa ni kama kuiaga Canada! Hakuamini kama wangerudi tena katika nchi hiyo ingawa hakuelewa ni kwanini moyoni mwake aliwaza hivyo. Walipotua Baghdad, Manjit alichukua teksi iliyowapeleka moja kwa moja hadi ofisini kwa Patrick, haikuwa shida kumwona kwa sababu alishawataarifu walinzi juu ya ujio wao.

“Pole sana Manjit kwa yaliyojitokeza lakini naamini yana mwisho wake!”

“Mungu anajua tu!”

“Habari za Canada?’

“Ndugu yangu ni kama Ulivyosikia!”

“Sasa itakuwaje katika deni lililobaki?”

“Hata mimi sifahamu maana pesa zote nilizokuwa nazo benki ndizo nilizokupa na sielewi  nitapata wapi pesa zaidi!”

“Unasemaje?” Aliuliza Patrick kwa hamaki.

“Kwa kweli sijui mahali pa kupata pesa zaidi!”

“Utalipa tu!”

“Patrick sina biashara nyingine yoyote, vituo vyangu vyote vya mafuta vimefungwa!”

“Hayo mimi hayanihusu utalipa tu sababu umejileta mwenyewe hapa Baghdad! Vinginevyo utaozea jela!”

“Patrick!!!!!!!!!!!!!!!!!!!”

“Nini?”

“Tafadhali nivumilie kidogo au nipe kazi yoyote katika kampuni yako ili niweze kulipa deni langu!”

“Haiwezekani hata kidogo ni lazima ulipe pesa!”Alisema Patrick akinyanyua simu yake.

“Hebu waambie hao vijana waingie upesi!”Patrick alisema na dakika kama  tatu baadaye mlango ulifunguliwa wakaingia vijana watano wenye nguvu  sawasawa na kuwakamata Manjit na Victoria! Wakaanza kuwavuta kuwatoa ofisini kwao Patrick.

“Hebu huyo mama mwacheni, mpelekeni kituo cha polisi huyo tapeli wa kimataifa, niachieni huyo mama hapa!”

“Sawa bosi!”

Victoria huku akilia machozi alirudishwa    na Manjit alitolewa hadi nje ambako alipakiwa ndani ya gari na safari ya kwenda kituo cha polisi ilianza haraka iwezekanavyo.

“Mama huyo kijana ni nani yako?”

“Ni mtoto wa dada yangu!”

“Dada yako mbona wewe mweusi yeye mchanganyiko?”

“Ni habari ndefu sana kijana,  ila ninaweza kukueleza ukitaka!”

“Nieleze bibi!”

“Niache  kwanza nipumzike, itanitia uchungu sana kuyaongelea mambo hayo,  naomba unitafutie chakula na mahali pa kulala  ili nipumzike  na ninachokuomba  sana usimfunge mwenzako ana matatizo makubwa  mno!”

“Hata mimi namhurumia bibi lakini baba yangu hataki kabisa, anadai deni hili limemuongezea ugonjwa wake!”

“Nipeleke mimi nikaongee naye labda atanielewa!”

“Sidhani!”

“Wewe nipeleke tu! Kwani baba yako anaitwa nani?”

“Anaitwa Abdulwakil

“Ni mwenyeji wa wapi?”

“Tanzania!”

“Tanzania? Alifikaje huku?” Aliuliza Victoria kwa mshangao.

“Ndiyo! Alikuja miaka mingi sana akiwa mtoto”

“Mbona hata mimi pia nilitokea Tanzania?”

“Kweli?”

“Ndiyo!”

“Basi si ajabu mtafahamiana!”

“Inawezekana!”

Victoria anapelekwa kukutana na Nicholaus bila kufahamu! Baad ya kupotezana kwa miaka mingi!

****

Tayari   Manjit alishaingia mikononi mwa polisi na alikuwa ndani ya gari akipelekwa kituoni, hiyo ilitokea baada ya kumweleza Patrick ukweli kuwa asingeweza  kumlipa pesa alizokuwa akimdai,Victoria  aliumia sana moyoni mwake wakati Manjit akiondolewa ndani ya ofisi ya  Patrick  huku akiliita jina lake, alishindwa angemsaidia vipi Manjit mtu pekee aliyekuwa akimtegemea kwa wakati huo.

Walitoka   ofisini  Patrick akiwa amemshika mkono Victoria na kumuongoza hadi mahali  lilipokuwa gari lake la  kifahari aina ya Potsche, na kuingia ndani, Patrick alikaa kwenye usukani na Victoria alikaa kushoto kwake, ilikuwa ni safari kwenda nyumbani kwa tajiri Abdulwakil ambako Victoria alikuwa akipelekwa  kuongea na tajiri huyo aliyemiliki visima vingi vya mafuta  ili ajaribu  kumshawishi asimfunge Manjit kwani ndiye alikuwa tegemeo lake maishani.

“Akiniona katika hali  hii ya upofu   ni lazima atabadili nia yake ya kumfunga Manjit, Mungu yupo pamoja na mimi ninaamini atanihurumia!” Aliwaza Victoria wakati gari likipita kwenye mitaa ya  katikati ya  jiji la Baghdad kuelekea nyumbani kwa tajiri Abdulwakil kilometa  kumi na tano nje ya jiji.

“Hivi  baba yangu atakubali kweli? Sina uhakika anachotaka yeye ni  pesa na kama hakuna pesa lazima Manjit atafungwa tu!”

“Mwanangu niache nikaongee naye akikataa basi lakini nitakuwa nimejaribu!”

“Sawa mama!”

Gari lilizidi kwenda kwa kasi na   dakika    kumi na tano baadaye  liliacha barabara na kukata kona kuingia kulia likipita chini ya miti mirefu, mbele zaidi kama nusu kilometa lilikata tena kushoto na kuzidi kutokomea ndani! Hatua kama mia mbili mbele Victoria alisikia honi ikipigwa na mlio wa geti likifunguliwa ulisikika, akafahamu walikuwa wamefika mahali walipokuwa wakienda.

“Asalam alekum!”

“Aleikum salam!”

Alisikia maneno hayo kila walivyozidi kusonga mbele hatimaye gari likasimama kabisa na Patrick alifungua mlango na kuzunguka hadi upande wa pili ambako pia alifungua mlango na kumsaidia Victoria kushuka.

“Tumefika!”

“Kumbe sio mbali?”

“Kwa kweli sio mbali sana!”

Patrick akiwa amemshika mkono Victoria waliongozana na kuanza kupandisha ngazi taratibu, aligundua walikuwa wakiingia ndani ya nyumba, kila mahali walikopita salamu zilisikika na milango ilifunguliwa na wakaingia hadi ndani ambako Victoria  alisaidiwa kuketi kitini.

“Karibu mama hapa ndio nyumbani kwetu!”

“Ahsante sana  mwanangu, kikubwa naomba   unisaidie nikutane na baba yako!”

“Basi nisubiri  hapa nikaongee naye” Alisema Patrick, alionekana  kumwonea huruma sana Victoria lakini hakuwa na uwezo wa kumsaidia kwa sababu mwenye amri alikuwa ni baba yake mzazi.

“Haina matatizo!” Aliitikia Victoria na  baadaye akasikia mlio wa viatu ukiondoka mahali alipokaa.

Alisubiri kwa muda mrefu mno bila Patrick kurejea, alishindwa kuelewa ni kitu gani  kilichokuwa kikiongelewa huko ndani! Hofu yake kubwa ilikuwa ni tajiri Abdulwakil kukataa kuonana naye alimwomba Mungu wake hilo lisitokee. Mawazo yake yote wakati akisubiri yalikuwa juu ya Manjit ambaye alikuwa polisi, hakujua ni kitu gani wangekuwa wamemtenda! Alizidi kumwomba Mungu amwepushe Manjit na mabaya yote, hakuwa tayari kushuhudia Manjit akipatwa na tatizo kwani maisha bila yeye yasingewezekana, alikuwa tayari kufa pamoja naye.

Baadaye akiwa sebuleni alianza kusikia minong’ono kutoka upande wa pili, ilikuwa ni sauti  nzito ya kizee ikifoka! Hakuelewa ni nini kilichokuwa kikiongelewa kwa sababu maongezi yalifanyika katika lugha ya Kiarabu.

Kadri  dakika zilivyozidi kwenda ndivyo sauti ya mzee akifoka ilivyozidi kuongezeka na kukikaribia chumba alichokuwa amekaa, hofu kubwa ilimpata moyoni mwake akijua kitu kibaya kilikuwa kikimfuata! Alianza kulia akimwomba Mungu abadilishe mawazo ya wabaya wake.

“Ee Mungu  wangu  naomba unisai……..!” Alisema Victoria  lakini kabla hajaimalizia sentensi yake mlango ulifunguliwa na nyayo za watu wengi zilisikika zikiingia, alikaa kimya akisubiri sauti ya Patrick iongee lakini badala yake alisikia sauti nzito ya mzee ikifoka.

“Yuko wapi huyo? Hawa watu wanafikiri sisi tunafanya mchezo na biashara, ikibidi hata  huyu mama tutamfunga pamoja na Manjit!” Alifoka mzee huyo, sauti yake pekee ilitosha kumtisha Victoria.

Victoria aliposikia kauli hiyo aliinamisha kichwa chake na kuuficha uso wake katikati ya miguu yake miwili, kwa maneno yaliyosemwa na mzee huyo alijua taabu kubwa ilikuwa inakuja! Aliumia sana moyoni mwake, alifikiri shida zilikuwa zimekwisha katika maisha yake kumbe haikuwa hivyo alitakiwa kupambana na matatizo mengine tena.

“Hebu mleteni hapa!” Aliamrisha mzee huyo na Victoria alibebwa juujuu na kupelekwa moja kwa moja hadi  mahali mzee huyo alipokaa.

“Nisamehe sana mzee, naomba   unisikilize kwanza ninachotaka kusema!”

“Onyesha uso wako kwanini unaficha sura? Hebu mnyanyueni sura yake niione  ingawa ukitaka kumuua nyani usimwangalie usoni!” Alisema tajiri Abdulwakil na vijana kama watatu walimshika Victoria shingoni na kuanza kukinyanyua kichwa chake.

“Khaa! Victoria ni wewe?” Tajiri Abdulwakil alisikika akipiga kelele.

Victoria alishangaa  kusikia mtu aliyemhofia  akimwita kwa jina, hakuwa maarufu kiasi cha kujulikana kwa tajiri Abdulwakil!

“Wewe ni nani unayeniita jina?”

Tajiri Abdulwakil hakujibu kitu kwa mshtuko alioupata alilegea na kuanguka moja kwa moja sakafuni! Ikawa hekaheka ndani ya chumba, watu wote hawakuelewa ni nini kimempata ikabidi kwa haraka haraka abebwe na kutolewa moja kwa moja hadi nje ambako alipakiwa ndani ya gari na kukimbizwa hospitali! Hakuna mtu aliyeelewa kilichotokea, kilibaki ni kitendawili.

“Au yule bibi ni  mchawi nini?” Aliuliza Patrick wakiwa  ndani ya gari kuelekea hospitali.

“Kwanini unafikiri hivyo Patrick?”

“Maana amening’ang’ania sana nimlete kwa baba sasa baada tu ya baba kumwona ameanguka na kupoteza fahamu. Kama  baba akifa  kwa hakika nitamuua huyu bibi kizee! Hawezi kuniulia baba yangu hivi hivi nikamwacha hai” Aliendelea kusema Patrick huku machozi yakimtoka.

Walipofika hospitali walipokelewa na tajiri Abdulwakil akiwa hajitambui alikimbizwa moja kwa moja hadi chumba cha wagonjwa mahututi, iligundulika baadaye kuwa mmoja wa mishipa yake katika ubongo ulipasuka sababu ya mshtuko mkubwa alioupata. Jambo hilo lilimfanya Patrick aamini  Victoria alikuwa na majini na alimpiga baba yake na moja ya majini yake.

“Nitamuua! Hakyanani nitamuua! Nikirudi nyumbani tu lazima afe na atafukiwa ardhini hakuna mtu atakayejua”

**************

Kwa sababu ya kuchanganyikiwa na tukio lililotokea Patrick alimsahau Victoria ndani ya nyumba yao na kuondoka mbio kwenda hospitali, alibaki sebuleni akiwa katika dimbwi la mawazo na maswali yasiyokuwa na majibu, alishindwa kuelewa ni nani  aliyemwita kwa jina, aliamini hapakuwa na mtu yeyote aliyemfahamu  katika nchi ya Iran.

Alivuta kumbukumbu zake kwa muda akijaribu angalau kuikumbuka sauti aliyoisikia lakini hakupata jibu na kilichomchanganya zaidi ni kitendo cha kumsikia  Patrick akimtupia lawama juu ya  matatizo yaliyompata baba yake! Aliogopa na kuamini lazima Patrick angemfanyia kitu.

Ni wasiwasi huo ndio uliomfanya atoke taratibu sebuleni na kutembea hadi nje akishika ukuta,  nyumba  nzima ilikuwa kimya  iliashiria watu wote hawakuwepo, aliamini wote walimkimbiza tajiri Abdulwakil hospitali.

Nyumba ya tajiri Abdulwakil ililindwa kila upande, ilikuwa si rahisi kutoka wala kuingia ndani  ya nyumba hiyo bila kuonekana lakini kwa tukio lililotokea siku hiyo, walinzi wote walikusanyika sehemu moja na kuanza kujadili juu ya kilichompata tajiri wao.

“Sijui kapatwa na nini?”

“Hata mimi sifahamu, nimeona tu akitolewa ndani na kupakiwa ndani ya gari na kwa haraka gari likaanza kuondoka!”

“Labda mama yumo ndani tumuulize?”

“Hata yeye hayupo amekwenda hospitali!”

“Atapona kweli mzee?”

“Kwa hali niliyomwona nayo kwa kweli nina wasiwasi!”

Wakati maongezi hayo yakiendelea Victoria alikuwa akiupapasa ukuta kwa kuuzunguka akitafuta mahali pa kutokea, alikuwa ameamua kutoroka kwenda mahali kusikojulikana, mwili wake ulihisi mabaya! Alijua kama Patrick angerudi kutoka hospitali na kumkuta ni lazima angemdhuru na hata kumuua kabisa, Victoria hakuwa tayari kwa hilo.

Alipapasa kwa  dakika ishirini nzima ndipo  akafanikiwa kulifikia lango, kubwa lilikuwa limefungwa lakini alipopapasa pembeni alifanikiwa kugusa kitu kama komeo, alipokishika na kujaribu kukifungua na kisha kuvuta   alishangaa kuona lango dogo likifunguka! Akamshukuru Mungu na kwa taratibu pamoja na uzee wake alinyata na kutoka nje bila kuonekana na mtu yeyote.

Sababu ya upofu alisimama bila kujua aelekee wapi, aliusikiliza moyo wake kwa muda na akakumbuka maneno aliyoambiwa kanisani  miaka mingi akiwa mtoto mdogo kuwa Mkono wa kulia ulikuwa mkono wa Kuume ambao uliaminika kuwa na baraka! Bila hata kujadili mara mbili Victoria alikata kulia  akachuchuma na kuanza kutambaa akielekea vichakani bila kujua  mahali alikokuwa akielekea.

Kwa saa nzima alitambaa ardhini akipita katikati ya nyasi zilizomuwasha mwili mzima,  hakujali kwa sababu alishaamua kujiokoa, machozi yaliendelea kumtoka sababu ya Manjit aliyekuwa polisi! Kwa mara nyingine alikuwa ametenganishwa na mtu aliyempenda na aliyekuwa msaada pekee kwake!Kumbukumbu zake zilimrejesha tena kwa kaka yake Nicholaus.

“Yaani kila mtu anayejitolea kunisaidia anaondolewa   kwangu! Wa kwanza alikuwa Nicholaus, akaja Leah, baadaye Manjit lakini  hata yeye wameninyang’anya! Nitaishije mimi  Victoria? Ni heri kufa  kuliko mateso haya!” Aliwaza akizidi kutambaa kwenda mbele zaidi katikati ya vichaka.

Mpaka masaa matatu baadaye alikuwa bado akitambaa  porini, alikuwa bado hajaonekana wala kukutana na mtu yeyote! Alimshukuru Mungu kwa hilo mbele zaidi alichoka na kuamua kulala chali ardhini na kuamua kuifungua ncha moja ya nguo aliyojifunga na kutoa kipande cha noti walichogawana na kaka yake, alikuwa bado akikitunza! Hakuwa tayari kukipoteza kwake ilikuwa ni bora apotee yeye lakini si kipande hicho cha noti alichokichukulia kama kaka yake.

“Hivi kweli ipo siku nitakutana na Nicholaus na kuiunganisha  noti yetu?” Aliwaza Victoria akiwa amelala chali ardhini, alikuwa amechoka hoi bin taaban na njaa ilimsumbua, si njaa tu kulikuwa na mbu wengi waliomuuma kila sehemu ya mwili wake, ingawa alikuwa kipofu  hali ilimuonyesha kuwa tayari  usiku  ulishaingia.

Hakuwa na matumaini ya kumwona Manjit tena!

*************

Taarifa za tajiri Abdulwakil kuanguka ghafla nyumbani kwake baada ya kumwona mwanamke mzee zilitapakaa kila sehemu ya mji wa Baghdad! Watu wengi walifurika hospitali kushuhudia kilichompata mtu  waliyeamini alikuwa tajiri kuliko wote nchini humo.

“Ni jini!”

“Kweli eh?”

“Hakuna kitu kingine! Si ajabu maadui zake walimtuma  bibi kizee nyumbani kwake wakiwa wamemvalisha jini chinjachinja!”

“Lakini kweli inawezekana!”

Hayo ndiyo yalikuwa maneno ya kila mtu aliyefika hospitali, hawakuruhusiwa kumwona mgonjwa watu wote waliongea na Patrick na kumpa pole na alivyowasimulia yaliyotokea wote waliamini bibi alitumwa.

“Huyo bibi yuko wapi?” Aliuliza mmoja wa wafanyakazi kwenye visima vilivyomilikiwa na tajiri Abdulwakil.

“Tulimwacha nyumbani!”

“Kwa hiyo atakuwa bado yuko nyumbani kwenu?”

“Naamini hivyo!”

“Jamaniee!” Alipiga kelele mfanyakazi huyo na wafanyakazi zaidi ya mia tatu waliokusanyika walikaa kimya kumsikiliza yeye, alikuwa ni kiongozi wao katika visima vya mafuta.

“Ni lazima huyu bibi tukamuue, hawezi kumuumiza tajiri yetu na ushirikina au mnasemaje?”

“Sawaaaaaaaaa!”Wafanyakazi wote waliitikia.

Kama walioamrishwa waliingia ndani ya magari yaliyokuja nayo kutoka kwenye visima vya mafuta na kwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa tajiri Abdulwakil kwa lengo la kwenda kumkamata Victoria na kumuulia mbali. Walipokelewa na walinzi na walipomuulizia bibi walinzi hawakuwa na jibu kwa sababu hawakutaarifiwa kuwa kulikuwa na mtu aliyebaki ndani ya nyumba!

“Ingieni muangalie!”

Kiongozi wa wafanyakazi  hao na wenzake wawili waliingia hadi sebuleni na kuanza kumsaka Victoria bila mafanikio,  walinyanyua hadi viti na meza na kumwangalia chini yake lakini bado hakupatikana.

Walitoka nje na kuwataarifu wenzao juu ya kutoonekana kwa mtu waliyekuwa wakimtafuta ndani ya nyumba, waliamua kuacha ili wafanye msako asubuhi iliyofuata, baadaye Patrick alirudi kutoka hospitali na kuungana nao! Yeye ndiye aliwajaza jazba zaidi wafanyakazi wake pale  alipowaeleza wazi kuwa  mwanamke aliyemsababisha baba yake  matatizo alistahili kufa.

Wafanyakazi walilala nje ya nyumba ya akina Patrick  na asubuhi ilipowadia, nyumba nzima kwa msaada wa Patrick ilianza kupekuliwa lakini mpaka hatua ya mwisho hawakuweza kumwona ndipo ukatolewa uamuzi watafutwe nje ya ngome.

“Hatakuwa mbali na hapa, si ajabu alifanikiwa kutoka na yupo porini!” Patrick aliwaeleza wafanyakazi wake, alikuwa amedhamiria kumuua Victoria kabisa akiamini alimpiga baba yake na jini! Hakuna mtu kati yao aliyeelewa kwanini Abdulwakil alipoteza fahamu mara tu baada ya kumwona mwanamke huyo na kilichowashangaza zaidi ni kitendo cha  Abdulwakil kumtaja mwanamke huyo kwa jina kabla ya kupoteza fahamu.

“Jamani hizi ni nyayo za nani? Lazima kuna kitu kimepita hapa kikijivuta!” Alipiga kelele mmoja wa wafanyakazi waliokuwa wakimsaka Victoria.

Mchana kabla   Victoria hajapelekwa nyumbani kwa tajiri Abdulwakil mvua kubwa sana ilinyesha ni hiyo ndiyo iliyofanya nyayo na alama za Victoria akitambaa ardhini zionekane.

“Ni yeye ndiye kapita hapa!”Patrick alisema na kuwaongoza wafanyakazi wake kuzifuata nyayo hizo porini,walitembea karibu masaa mawili wakizifuata nyayo hizo porini, ghafla walimsikia mtu aliyekuwa mbele yao akipiga kelele kwa sauti.

“Huyu hapa! Huyu hapa!” Wafanyakazi wote walikimbia kwenda mbele kila mtu na silaha yake, mwenye rungu, mwenye jiwe, mwenye panga, mwenye nondo tayari kwa kumuua Victoria.

Alikuwa usingizini lakini kelele hizo zilimzindua alishindwa kuelewa ni akina nani waliokuwa wamemzunguka.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatatu hapahapa.