
JESHI la Zimamoto na Uokoaji (FRF) linatazamia kujizatiti kupanua wigo wa utoaji huduma kwa jamii.
Hayo yamesemwa leo na Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, Dk Thobias Andengenye wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam ambapo alisema katika utekelezaji wa zoezi hilo, jeshi lake limedhamiria kufanya klabu mbalimbali za zimamoto na uokoaji sehemu mbalimbali nchini ikiwemo mashuleni na maeneo mengine.
Alisema kuwa katika klabu hizo wataweza kutoa elimu juu majanga ya moto yanayoweza kutokea na kwamba elimu hiyo kuhakikisha inapokelewa kwa kiwango cha kuridhisha.
Aidha katika taarifa yake, alibainisha baadhi ya changamoto wanazokutana nazo kuwa ni pamoja na ucheleweshwaji wa kupata taarifa za ajali za moto, jambo linalodhorotesha huduma za jeshi hilo.
”Changamoto ya barabara imekuwa sababu nyingine ya kutofika kwa wakati kutokana na watumiaji wengine wa barabara kutotii na kutambua umuhimu wao,” alisema.