
Na AMANDA POSH| MAHUSIANO| MAKALA
MPENZI msomaji, karibu tena kwenye safu hii bora kabisa ya Sindano za Mastaa. Wiki iliyopita ulikuwa na staa wa Bongo Fleva, Athuman Omary ‘Harmorapa’ ambaye kila siku amekuwa akitengeneza vichwa vya habari kutokana na matukio yake. Wiki hii unakutana na msanii wa Bongo Muvi, Tamrinah Mohamed Poshi ‘Amanda’ aliyebarikiwa figa bomba na matata ambaye anafunguka kuwa, usaliti ni sumu mbaya na hatari mno kwenye uhusiano. Tambaa naye sasa…
PENZI HALIGAWIKI
Jamani mashabiki wangu wazima? Tukiingia moja kwa moja kwenye mada ya leo, mnapaswa kufahamu kwamba, hakuna mtu anayependa kuchangia penzi na mtu mwingine. Si mwanaume wala mwanamke.
Hakuna anayetaka penzi lake ligawanyishwe kwa mtu mwingine. Kama ndivyo, kwa nini baadhi ya wanaume mnawasaliti wapenzi wenu? Kwa nini mnawaumiza wapenzi wenu ambao mmewatafuta na kuwagharamikia vitu vingi, ikiwemo muda, mali na vinginevyo?
UNAKOSA NINI?
Huwa najiuliza, hivi ni kitu gani mwanaume unakosa kwa mpenzi wako kiasi cha kuamua kumsaliti mtu anayekupenda? Mapenzi yanauma sana, ila usaliti unauma zaidi, ni doa na sumu mbaya sana kwenye uhusiano. Bila shaka hakuna mtu anayependa utamu wake uonjwe na mtu mwingine ndiyo maana kila siku tunasikia, wapenzi wameuana, mpenzi ameua, amefungwa, amefumaniwa, amepigwa na mambo mengine mengi, kisa kupinga kuonjwa kwa utamu wa mtu.
UPENDO HUPUNGUA
Mwanamke au mwanaume ambaye hana tabia za kuchepuka, mvumilivu, mwenye upendo kwa mwenza wake, siku akibaini kuwa mpenzi wake anamsaliti, moyo wake hupoteza upendo wa zamani aliokuwa nao.
AMANI HUTOWEKA
Usaliti huohuo husababisha amani kutoweka ndani ya nyumba, kwa sababu mwanamke au mwanaume anafahamu kabisa kuwa mpenzi wake anam’cheat’ lakini yeye anakataa katakata. Kinachofuatia ni mwanamke kutokuwa na imani na mumewe au mpenzi wake, hata kama akiaga kiukweli kuwa anakwenda msibani, basi mwanamke atahisi tu kuwa anakwenda kuchepuka. Hii ni hatari sana.
KUTOKUAMINIANA
Ninaposema ni doa na sumu katika mapenzi, namaanisha uchepukaji au usaliti husababisha kutoweka kwa uaminifu baina ya wapenzi. Kila mmoja huwa hana imani na mwenzake. Mtindo huo husababisha kuzalisha;
CHUKI
Usaliti ukiendelea, huzalisha chuki baina ya mtu na mpenzi wake. Mwanamke huwa haoni tena thamani ya kumuandalia chakula mezani mpenzi wake kwa sababu anajua ni kama dharau, yaani atoke kwa mwanamke mwingine halafu yeye ndiye amuandalie chakula? Haiwezekani!
USALITI HUIBUKA
Baada ya chuki kukolea na kujengeka ndani ya moyo wa msalitiwa basi hujenga tabia ya ujasiri wa usaliti na hapo ndipo naye huamua kwa sababu mpenzi au mwenza wake anachepuka, basi na yeye anaanza kuchepuka. Unadhani nini kitafuatia baada ya wapenzi kuanza kufanyiana visasi vya mapenzi, mwisho wake bila shaka, hautakuwa mzuri zaidi ya kutengana.
Kama kweli unahitaji kuingia kwenye uhusiano wa mapenzi, tafuta mtu mmoja ambaye utampenda kwa dhati na kwa hali na mali. Kwa maoni na ushauri, tembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Amani kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Insta: mimi_na_uhusiano au unaweza kujiunga na M&U WhatsApp kupitia 0679979785