
Msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya kutoka Kundi la Weusi, Rapa Nikki wa Pili amewafungukia wasanii wa filamu za Kibongo kufuatia kitendo chao cha kuandamana hadi Kariakoo hivi karibuni, wakishinikiza filamu za nje zizuiwe ili filamu zao zipate soko.
Kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii, Nikki wa Pili amesema wasanii wenyewe wa Bongo Movie ndiyo waliosababisha filamu zao kukosa soko kwa sababu wengi wao wanafahamika kwa mambo mengi tofauti na kazi zao za sanaa.
Akaeleza kwamba mwanzoni mwanzoni, wasanii wa Bongo Movie walifanikiwa kuliteka soko la filamu lakini kilichowashinda ni kuendelea kudumu kwenye soko kwani kazi walizokuwa wakizifanya awali, zilikuwa na tija kwa wananchi, tofauti kabisa na wanazozifanya sasa.
“Bongo movies mwanzoni walikuwa na soko, kuanza ni kujaribu, ila kudumu kunahitaji sayansi ya hali ya juu… mwendelezo wa lolote huhitaji maarifa…” alisema.

Nikki aliongeza kuwa, maisha binafsi ya baadhi ya waigizaji wa Bongo Movie, yamewafanya watu wengi kutofuatilia kabisa kazi zao, kutokana na kukosa maadili kuanzia kwenye maisha binafsi mpaka kwenye kazi zao.
Akaongeza kuwa hakuna uhusiano wowote katika maisha ya wasanii hao na kazi zao, jambo linalosababisha watu kushindwa kuwaamini pale wanapowaona wakiigiza filamu zao.
“Movies za Rambo ni maarufu kuliko Rambo mwenyewe, Bongo movies tunawajua kwa vitu vingine zaidi wala hata siyo movie zao,” alisema Nikki wa Pili.
Akaongeza kueleza kwa kumtolea mfano mcheza filamu maarufu wa Hollywood, Denzel Washington kwamba maisha yake halisi ya kila siku, yanakufanya hata unapotazama movie zake, uamini kwamba kile anachokiigiza kina uhalisia.
“Nampenda Denzel kwenye movie na kwenye maisha ya kawaida, kwenye interview, kwenye speech, anajua kukufanya uamini movie zake,” alisema Nikki wa Pili.
Hiki ndicho alichokiandika kupitia kurasa zake za kijamii katika mitandao ya Twitter na Instagram.

