
MSIMU wa 2016/17 wa Ligi Kuu Tanzania Bara umefika tamati wiki iliyopita huku timu ya Yanga inayonolewa na Mzambia, George Lwandamina ikifanikiwa kutetea ubingwa wake kwa mara ya tatu mfululizo.
Yanga wamenyakua taji hilo wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa na wapinzani wao Simba huku timu zote zikimaliza ligi zikiwa na pointi 68 baada ya mechi 30.
Ukiondoa ubingwa huo wa Yanga ambao ni rekodi, kuna matukio ambayo yamejitokeza na yameacha gumzo ndani ya msimu huu

Sakata la kadi ya Fakhi
Hili ndilo linaweza kuwa gumzo katika msimu huu kwani liliibua sintofahamu ya aina yake na ilikuwa ikifuatiliwa na kila shabiki wa soka kutokana na mwenendo wake ulivyokuwa.
Ishu nzima ilianza muda mfupi baada ya timu ya Simba kupoteza mechi yake dhidi ya Kagera Sugar kwa mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Kaitaba, ambapo baada ya mechi hiyo kuisha viongozi wa Simba waliibuka na hoja ya kumkatia rufaa beki wa Kagera, Mohammed Fakhi wakidai alicheza mechi hiyo akiwa na kadi tatu za njano.

Baada ya kukata rufaa hiyo, Kamati ya Saa 72, iliwapa Simba pointi tatu baada ya kugundulika Fakhi ana kadi tatu za njano kabla ya baadaye maamuzi hayo kubatilishwa na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ambayo ilikuja kuzipoka pointi hizo ambazo zimewafanya viongozi wa Simba kupeleka shauri lao kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) wakidai kutotendewa haki.
Idadi kiduchu ya mabao
Msimu huu unaonekana kuwa mgumu baada ya idadi ya mabao kupungua kuanzia kwa mfungaji bora msimu uliopita Amissi Tambwe aliyemaliza akiwa na mabao 21 lakini msimu huu mfungaji bora ana mabao 14 pekee.
Lakini suala hilo limeendelea zaidi hata kwa wachezaji ambao wamefunga mabao matatu ‘hat trick’ ambapo tofauti na msimu uliopita kuwepo sita msimu huu kuna hat trick mbili pekee.

Wazawa waamka kwenye ufungaji
Tofauti na msimu uliopita ambao ulitekwa na wageni katika ufungaji bora, msimu huu wazawa wameinuka na kupambana vilivyo kuhakikisha tuzo ya ufungaji haipandi ndege na wamefanikiwa juu ya hilo.
Kwenye ufungaji, Simon Msuva wa Yanga na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting wameibuka vinara wakifunga mabao 14 kila mmoja huku Mbaraka Yusuph, Shiza Kichuya na John Bocco nao wakifanya vyema katika kuwatungua makipa.

Kuvurugwa ratiba
Hili linaonekana kuwa tatizo sugu kwa sasa baada ya kujirudia tangu msimu uliopita, ambapo mara kwa mara ratiba imekuwa ikipanguliwa kwa baadhi ya mechi zake kutolewa siku husika kwa kupelekwa mbele au kurudishwa nyuma.
Katika kuonyesha waandaaji wa ratiba walichemka kwa kiasi kikubwa, hata fainali ya Kombe la FA kati ya Simba na Mbao iliyopangwa kupigwa Mei 28, imerudishwa nyuma hadi Mei 27, bila ya kuwepo kwa sababu maalumu.
Waamuzi kufungiwa
Hili nalo haliwezi kusahauliwa katika msimu uliopita baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwatupa korokoroni waamuzi wake kutokana na maamuzi mabaya kwenye mechi mbalimbali.
Waamuzi kama Martin Saanya, Rajabu Mrope walikutana na rungu la kufungiwa baada ya maamuzi mabaya ambayo waliyatoa kwenye baadhi ya mechi zao.

Uwanja wa Taifa kufungwa
Msimu umemalizika huku tukishuhudia Uwanja wa Taifa ukifungwa kwa muda baada ya kutokea vurugu zilizosababishwa na mashabiki wa timu za Simba na Yanga wakati timu hizo zilipopambana kwenye mzunguko wa kwanza.
Serikali ndiyo iliufunga uwanja huo kutotumika kwa Simba na Yanga ambazo ndizo zilikuwa zikiutumia kwa mechi zao za nyumbani kutokana na mashabiki wao kufanya uharibifu.
Katazo hilo baadaye lilikuja kulegezwa na hatimaye ukaendelea kutumika.

Manara afungwa mdomo
Imezoeleka waamuzi, makocha na wachezaji wa timu fulani ndiyo wanafungiwa kutokana na kukiuka sheria za soka lakini safari hii jumba bovu lilimuangukia Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara baada ya kufungiwa kujihusisha na soka kwa mwaka mmoja sambamba na faini ya Sh milioni tisa.
Hayo yote yalikuja ikiwa ni siku chache baada ya kutoa lugha kali kwa viongozi wa TFF, akidai wanaionea timu hiyo kwa kutoipa haki pale wanapopeleka malalamiko yao mara kwa mara.