
IKULU, DAR ES SALAAM: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo Jumatano, Mei 24, 2017 amepokea rasmi Ripoti ya Kamati Maalum ya Utafiti wa Mchanga (Makanikia) uliomo kwenye makontena yaliyozuiliwa kwenye bandari tofauti hapa nchini.
Akikabidhi ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo amemueleza Rais Magufuli kuwa makontena yaliyofanyiwa utafiti ni 277 ambapo Kamati yake imebaini kuwepo na ufisadi mkubwa kwenye suala la usafirishaji wa mchanga huo, ambapo kiwango kikubwa cha dhahabu kimekuwa kikitoroshwa kwenye mchanga huo.
“Kamati imebaini kuwapo kwa kiwango kikubwa cha dhahabu kwenye makontena ambapo kontena moja lina wastani wa kilogramu 28 za dhahabu ambapo thamani yake kwenye makontena zaidi ya 277 yaliyozuiwa bandarini ni kati ya Tsh bilioni 676 hadi trilioni 1.14.”
“Makinikia hayo yalikutwa pia na madini ya shaba, silva, chuma na shaba. Kiwango cha Silva kilikuwa 6kg-7kg kwa kontena moja hivyo kufanya jumla ya 1689kg kwa makontena 277 yaliyozuiwa bandarini.”
“Licha ya madini mkakati (strategic metals) kuwapo katika makinikia, hazikuwa zikifahamika na kusababishia serikali hasara.”
“Kamati imesema mashine ya ukaguzi wa makontena ina matatizo kwani walificha chuma ndani ya makontena na mashine haikuona. Sababu mashine za ukaguzi bandarini hazifanyi kazi vizuri, huenda njia hiyo ilitumika pia kutorosha meno ya tembo.”
“Kamati imependekeza makontena yapimwe vizuri ili kuweza kubaini aina na thamani za madini yote yaliyomo kwenye mchanga.
Kamati imependekeza watumishi wa TMAA na Wizara husika wanaohusika na upotevu wachukuliwe hatua.” alisema mwenyekiti huyo.
Ambapo baada ya hapo Mwenyekiti wa Kamati alimkabidhi Rais Magufuli nakala 5 za ripoti ambapo amemwambia baadhi ya mambo akiyasoma yatamkera.