
Stori: Gladness Mallya |Risasi | Habari
DAR ES SALAAM: Imevuja! Ile ndoa ya staa wa filamu za Kibongo, Sabrina Rupia ‘Cathy’ na mumewe Salim Rupia inadaiwa kuvunjika na sasa yupo anahangaika kuwalea wanaye watatu peke yake, Risasi Mchanganyiko limedokezwa.
Chanzo makini ambacho kiko jirani na anapoishi msanii huyo maeneo ya Kijichi, Dar, kilieleza kuwa ndoa ya muigizaji huyo imevunjika kwani mumewe aliondoka nyumbani hapo yapata miaka miwili iliyopita na hajarudi huku Cathy akidaiwa kusingizia kuwa mumewe amehamia Zanzibar kikazi. “Jamani hivi mna habari kuwa ndoa ya Cathy imevunjika muda mrefu na mumewe amemwachia nyumba anaishi na watoto wake tu, ndiyo maana hata haonekani akijiachia kama zamani na hiyo sasa hivi ndiyo habari ya mjini huku Kijichi nzima,” kilisema chanzo.

Baada ya kupata habari hizo, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Cathy na kuomba kuonana naye, lakini alikataa na alipoelezwa kuhusu madai hayo, aligeuka mbogo; “Kwani wanaoachika ni wadudu jamani, naombeni mniache, kuachika ni jambo la kawaida sana kwa kuwa sijazaliwa naye,” alisema kwa kifupi na kukata simu. Wawili hao walifunga ndoa miaka 15 iliyopita. Mara kwa mara muigizaji huyo ambaye huonekana katika viwanja vya kujirusha akiwa peke yake, akiulizwa kuhusu alipo mumewe, hudai yupo Zanzibar kikazi.