
MAKALA: BONIPHACE NGUMIJE
HIVI karibuni wakati nikipitia Mtandao wa Kijamii wa Instagram nilikutana na kitu kilichonifurahisha. Kilikuwa ni kipande cha video kilichokuwa kimerekodiwa na Mwanauziki wa HipHop Bongo aitwaye Songa.
Songa alikuwa akichana mistari iliyosikika;
‘Songa kumuiga 50 huwa siziwezi hizo busness, mi’ Magufuli mzee wa kazi so usinicheki niko bize, najiuliza hiki kizazi cha mafake nikimalize maana wanatema yai vipi chipsi niziagize, hii ni live kama FNL ya Sammy Misago, wana siwaelewi sijui wanampa salamu kinyago, nafahamu michapo siwezi kufanya usahau kichapo, je utaweza Bongo ikiwa ulishindwa kurap Chicago?
Baada ya kumsikiliza Songa vizuri nilitabasamu. Nikawaza kwa nguvu; ‘jamaa pia kaingia kwenye hii bifu’. Niliwaza kaingia kwa sababu nilijua wazi anawadis Godzilla ‘King wa Salasala’ na Wakazi ‘Swagga Bovu’ wasanii wenzake wa Hip Hop, ambao wapo kwenye bifu kali la kupimana uwezo. Kila mtu akijiona mkali kuliko mwenziye.

Kuna watu wanaweza kujiuliza nilijuaje anawadis! Lakini kwa mchanganuo ni kwamba mkali huyu wa Wimbo wa Mwendo Tu aliposema ; ‘Songa kumuiga 50 huwa siziwezi hizo busness’ –hapa alikuwa akimdis Godzilla ambaye staili yake ya kurap na swaggz zake huwa anarap kama Mwanamuziki wa Marekani, 50 Cent.
Akasema tena; ‘najiuliza hiki kizazi cha mafake nikimalize, maana wanatema yai vipi chipsi niziagize’ – hapa Songa alikuwa anawadis Godzilla na Wakazi kwa pamoja kutokana na tukio la hivi karibu baada ya washikaji hao kukutana katika ‘interview’ kwenye kipindi cha Bongo Dote Home cha Redio Times.
Wakiwa kwenye mahojiano Godzilla alikuwa akitema ‘yai’ muda mwingi jambo ambalo lilionekana kumkera hata mtangazaji wa kipindi hicho aliyemwambia Godzilla baadhi ya wasikilizaji wake watakuwa hawamuelewi.
Lakini kama haitoshi Wakazi pia alionyesha umwamba wake wa kufahamu lugha hiyo ya kigeni na kuanza kutema yai pia huku akijisifia kwamba Godzilla hamuwezi. Lakini pia kamchana kwenye ‘dis track’ yake mpya iitwayo Zillnass- kuwa Godzilla hawezi yai kama yeye maana anamatatizo ya ‘l’ na ‘r’.
Hiyo ni baadhi tu ya mifano kutoka kwenye mistari ya kipande hicho cha video ya Songa ambaye kwa anayewafuatilia wawili hawa anafahamu hata kwenye mstari wa mwisho Songa alikuwa anamdis Wakazi ambaye amewahi kuishi Chicago, Marekani.
Hata hivyo, bifu la Godzilla na Wakazi ambalo lilianzia kwenye Mtandao wa Kijamii wa Twitter kwa kujibishana maneno ya ‘mimi mkali kuliko wewe’ ‘huniwezi’ ‘swaga zako unaiga’ limeleta ladha fulani na msisimko kwenye Muziki wa HipHop, Bongo. Gemu lilikuwa limelala kwa muda maana nakumbuka miongoni mwa bifu ambalo limepata ‘airtime’ hivi karibuni ingawa si kihivyo ni la Nay na Madee ambao nao vita yao ni yakila mmoja kujiona mkali.
Kwa upande wa hawa washikaji wawili, tukianza na Wakazi anaamini Godzilla ameishiwa. Ana stress na kiti chake kimekaliwa na Mwanamuziki Billnass maana hatakwenye wimbo wake aliomdis Godzilla amesema kwa yai kuwa; ‘The crown shifted from Zilla to Billnass.’
Lakini Godzilla yeye anaamini ni mkali kuliko Wakazi na anamzidi kwa mengi. Pia katika wimbo wake mpya wa kumdis Wakazi uitwao Power amemchana mshikaji huyo kuwa bado mtoto kwenye gemu na kabla hajaingia kwenye gemu alikuwa akimuona yeye kwenye televisheni amekwisha kuwa staa.
Wote wanajiona wakali. Ingawa kuna baadhi ya vitu ukianza kuvichambua utaona kabisa wazi kuna sehemu Godzilla atafunikwa kama asipokuwa makini.
Binafsi nimesikiliza ‘interview’ zao ambazo wamefanya tangu wawe kwenye bifu. Kikubwa nilichogundua ni kwamba wakazi yupo ‘smart’ kwenye vitu vingi. Anatumia weledi kujibu maswali lakini hata kwenye kufreestyle mistari yake inaeleweka kuliko mfalme waSalasala.
Lakini pia sikilizia nyimbo zao.
Utaona Wimbo wa Zillnass wa Wakazi ni wimbo uliopangwa vizuri na unaeleweka kuliko Power wa Godzilla.
Kwenye Wimbo wa Power kuna sehemu Godzilla anaimba kuwa; “Asubuhi tunaamka tunasema Good mornning, Kifaransa ninakupa bonsoir ‘ – kitu ambacho si kweli. Kwa Kifaransa ‘bonsoir’ ni salamu ya jioni na angalau ‘bonjour’ ndiyo salamu inayoweza kutoka asubuhi. Japo si rasmi maana bonjour unaweza kuitoa pia muda wowote ule lakini pale unapomuona mtu kwa mara ya kwanza katika siku husika.
Kwa hiyo unaweza kuona ambavyo Godzilla hakuwa amejipanga.
Mbali na hayo yote bifu hili ‘kununuliwa’ na kituo cha runinga cha kimataifa cha MTV Base ni sawa na kulimaliza kiaina. MTV Base kupitia Mtandao wao wa Twitter walihitaji kukata ubishi kwa mashabiki wa wakali hawa kupiga kura ili kumpata rapa mkali kuliko mwenziye.
Utaratibu wa kura ulitakiwa kufanyika ndani ya saa 24, ambapo katika saa 14 za mwanzo Wakazi alikuwa anaongoza kwa asilimia 74 huku Godzilla akiwa na asilimia 26 tu za kura zote! Jambo lililoonesha Wakazi yupo mbele ya Zilla.
Kwa upande wa Billnas ambaye kahusishwa katika bifu hili na Wakazi kuwa anampa stress Godzilla yeye amesema hahusiki kwenye lolote katika bifu hilo na hafi kirii kuwa anampa stress Godzilla ingawa pia kaipongeza ngoma ya Wakazi kuwa ni nzuri. Lakini kwa namna fulani kajitoa kuhusishwa moja kwa moja kwenye hilo bifu lao.