
IKIWA ni siku mbili tangu ateuliwe kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, aliyekuwa Mkuu wa Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Mohamed Mpinga ametoa shukrani nyingi kwa Watanzania kufuatia ushirikiano waliompa katika kipindi chote alichoongoza nafasi nafasi hiyo.
Akizungumza na Global TV Online mapema leo ofisini kwake, Naibu Kamishna Mpinga amesema amepata ushirikiano mkubwa mno kutoka kwa wananchi wa sehemu mbalimbali nchini, ambapo walimtaarifu mambo mengi ya kiusalama wa barabarani, hivyo kurahisisha utokomezaji wa majanga mengi ya kiusalama wa barabarani.
Pia, Kamanda Mpinga alitumia fursa hiyo kuwashukuru wakazi wa Kanda Maalum ya Kipolisi ya Dar es Salaam kwa umoja na mshikimano katika kipindi chote cha utumishi wake, kama mkuu wa kitengo hicho. Aidha, alivishukuru vyombo vyote vya habari kwa kazi kubwa ambayo vimekuwa vikifanya kuhakikisha usalama barabarani unakuwa katika hali inayohitajika, licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali.
“Nawashukuru mno Watanzania wote kwa ushiriukiano wao katika kipindi chote ambacho nilikuwa katika nafasi hii ambayo naiacha sasa, lakini pia hata wakazi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam na bila kusahau vyombo mbalimbali vya habari, husasan Global TV Online ambao tumefanya kazi nyingi zaidi na mwisho nitoe wito wa kumpa ushirikiano wa kutosha huyu anayechukua nafasi yangu, lakini najivunia sana kwani wananchi wengi wamekuwa wakipigia simu akieleza raha ya usafiri ilivyotengamaa, Mungu awabariki sana,” alisema Kamanda Mpinga.