×

Ustaadh: Wadau wanataka ndonga zipigwe Jumapili

Rais wa TPBO, Yassin Abdallah ‘Ustadh’ akiwatambulisha mabondia Idd Pialali wa Tanzania na Regin Champion wa Congo.

 

WAKATI zikiwa zimebaki siku nne, Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO) chini ya rais wake, Yassin Abdallah ‘Ustaadh’ imesema kuwa wameamua kupeleka mbele mapambano ya Kimataifa ya Ubingwa wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati kufuatia kupokea maombi mengi ya wadau kutoka ndani na nje ya nchi.

 

Mapambano hayo ambayo yatawakutanisha mabondia watatu wa Tanzania dhidi ya wenzao kutoka Malawi, Zambia na DR Congo ambapo awali yalipangwa kufanyika Julai 22 kabla ya kusogeza mbele na sasa yatapigwa Julai 23, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Dar Live, Mbagala Zakhem jijini Dar.

 

Akimtambulisha bondia Israel Kamwamba – Malawi.

 

Katika mapambano hayo ya kimataifa, yaliyoandaliwa na kampuni ya kupromoti mchezo wa ngumi za kulipwa nchini, Solid Rock Tanzania ambayo yatasim-amiwa na TPBO huku yakirushwa mubashara na Kituo cha Global TV Online kupitia website yake ya www. globaltvtz.com.

 

Tanzania itawakilishwa na Francis Miyeyusho ‘Chichi Mawe’, atakayezichapa dhidi ya Israel Kamwamba kutoka Malawi, Nasibu Ramadhani ‘Pacman’ anatarajia kuonyeshana umwamba ndani ya ulingo na Mzambia, Benard Mwanga huku Idd Pialali akitarajia kupeana vitasa vya aina yake na Regin Champion raia wa DR Congo.

Francis Miyeusho ‘Chichi Mawe’ -Tanzania.

 

Ustaadh amesema kuwa wamepokea maombi mengi kutoka kwa mashabiki wakitaka mapambano hayo yapigwe Jumapili badala ya Jumamosi kitu ambacho wamekipitisha kwa moyo mmoja ili kuweza kutoa nafasi kubwa kwa wadau kushuhudia mapambano hayo ‘live’ kupitia Global Tv Online.

 

“Baada ya kuwatangaza mabondia kutoka Malawi na DR Congo wakiwa na mabondia wa hapa wikiendi iliyopita kwa ajili ya mapambano yetu ya Ubingwa wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati, tulianza kupokea simu nyingi na meseji kutoka kwa wadau wakiomba mapambano yafanyike Julai 23 badala ya 22 kama ilivyopangwa.

 

“Sasa kutokana na mwitikio wao kuwa mkubwa sisi kama TPBO ambao ni wasimamizi pamoja na muandaaji na mdhamini Global TV, tumeona ni vyema tukazi-ngatia maoni ya mashabiki na wadau kwa jumla kwa sababu simu kutoka Malawi, Zambia, DR Congo, Afrika Kusini, Uingereza na Marekani zilikuwa nyingi na wote hao wakitaka kuwa hivyo.

“Nichukue fursa hii kuwaambia wadau na Watanzania kuwa mapambano yetu ya ubingwa wa Global TV yatapigwa Siku ya Jumapili, zimebaki siku nne kuanzia leo yaani wikiendi hii lakini nje ya hapo kesho Alhamisi tunatarajia kumpokea bondia kutoka Zambia Benard Mwanga, ataingia usiku wa kesho hivyo atakamilisha idadi ya mabondia watatu kutoka nje.

 

“Tumewasiliana naye akiwa katika maandalizi yake, kikubwa alichokisema anakuja kumuua mpinzani wake Nasibu Ramadhani kwa sababu anadai kinachomleta Bongo ni kuchukua Ubingwa wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati na siyo kuuza sura.

 

“Unajua bondia wetu hatakiwi kufanya masihara na huyu mtu maana siyo wa mchezo hata kidogo, tumefanya hivi baada ya bondia aliyetakiwa kucheza naye kutoka Zimbabwe, Tinashe Mwadziwana kuumia wakati akiwa mazoezini.

Mikanda ya Ubingwa.

 

“Lakini kwa upande mwingine mashabiki wanachotakiwa kufanya hivi sasa ili kuweza kuona mapambano hayo kwa njia ya simu au kompyuta, tena bure ambayo yatakuwa live wahakikishe wanajiunga (SUBSCRIBE) na YouTube Chanel ya Global TV Online sasa hivi. Yaani wanatakiwa kuingia YouTube halafu wanatafuta GLOBAL TV ONLINE, kisha wabonyeze neno subscribe, pia wabonyeze kikengele kidogo kilichopo pembeni yake ambacho kitawakumbusha kuangalia pambano hilo mara tu litakapoanza.

 

“Kama watakuwa wameshajiunga, basi wahakikishe pia wawe wamebonyeza kikengele ili wasipitwe na kila kitu kinachoendelea Global TV lakini wanaweza kuipata kupitia Mtandao wa www.globaltvtz. com , wajiunge sasa na Global TV ili wawe wa kwanza kuona ndonga za kihistoria hapa nchini. Wajiunge kwa kuingia www.youtube.com/user/uwazi1,” alisema Ustaadh.

 

Katika hatua nyingine, mapambano hayo, hayatakuwa na kiingilio na mashabiki wataweza kulishuhudia mubashara kupitia simu zao za mkononi tu, kwani litaonyeshwa na Global TV pekee.

Leave a Comment