×

VIDEO: Mjeda Apigwa Avunjwa Goti

Koplo Deus Kakuba, wakati alipokuwa akilitumikia Taifa.

 

MJEDA mmoja ambaye ni mwanajeshi mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Koplo Deus Kakuba Mkazi wa Chalinze yuko hoi kitandani akiugulia maumivu kufuatia kuvunjwa goti baada ya kupigwa na watu aliokuwa akilumbana nao.

 

Akizungumzia mkasa huo kwa masikitiko, Kakuba ambaye kwa sasa ni mlinzi wa Kampuni ya Knight Support alisema Julai 5, mwaka huu akiwa eneo lake la kazi maeneo ya Pingo, Chalinze walitokea walinzi wenzake wa kampuni nyingine wakiwa wamebeba mabomba, wakawa wanataka kuyapitisha kwenye lindo lake.

 

“Kitendo hicho nilikikataa kwa kuwa yale mabomba nilishahisi huenda yalikuwa ya wizi hivyo nilishikilia msimamo wangu wa kuwazuia kupita eneo langu,” alisema.

Akifafanua zaidi, Kakuba alikuwa na haya ya kusema:

 

Mguu uliojeruhiwa.

 

“Kitendo hicho kilionekana kuwakera wale waliokuwa na yale mabomba ambapo waliyashusha na kuanza kunipiga huku wakiwaita wenzao.

“Ndani ya kipindi kifupi waliongezeka na kuwa wengi nami nilikuwa peke yangu hiyo waliweza kunidhibiti na kunipiga na kunidhalilisha sana.

 

“Wakiwa wananisulubisha nilimsikia kiongozi wao akiwaambia wanipeleke kichakani waniue kisha waniweke hayo mabomba halafu wakija watu wawaambie mimi nilikuwa mwizi niliyeiba hayo mabomba ndiyo maana wameniua.

“Hapo nilikiona kifo kiko mbele yangu, nikiwa nimechoka sana yule kiongozi wao alinichukua na kuniingiza kwenye kichaka ambapo alinifanyia mambo ya kudhalilisha sana ambayo siwezi kuyaweka hadharani.

 

…Akiwa amejilaza.

 

“Nikiwa na huyo kiongozi wao wakatokea wenzao wengine ambao walimuonya yule kiongozi kuwa mambo anayonifanyia yanaweza kumgeukia na kumuingiza kwenye matatizo ndipo akaamua kuniacha lakini wakati huo alishanipiga na kitako cha bunduki na kunivunja goti.

“Jambo la ajabu walinichukua na nikiwa njiani nilipoteza fahamu kutokana na maumivu na kipigo, waliwapigia simu polisi ambao walinichukua na kunipeleka Kituo cha Chalinze na kunifungulia kesi ya wizi wa yale mabomba.

 

“Nilikaa hapo kituoni siku nne ndipo akatokea mwanangu anayesoma kidato cha tatu shule ya bweni na kuniwekea dhamana kwa kuwa mke wangu alikuwa safarini Mwanza na sasa natafuta wanasheria ili waweze kunisaidia.”

Kufuatia sakata hilo gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Jonathan Warioba kujua kinachoendelea katika sakata hilo lakini simu yake iliita bila kupokelewa.

 

STORI: Richard Bukos na Issa Mnally | UWAZI| Pwani

 

SHUHUDIA VIDEO AKISIMULIA

Leave a Comment