JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limepiga marufuku maandamano, maombi na mikusanyiko isiyo halali huku likielekeza kuwa iwapo mtu anataka kufanya maombi basi aende maeneo maalum ambayo ni kanisani au msikitini.
Hayo yamesemwa leo jijini na Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar, Lazaro Mambosasa alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa habari wakati akitoa ripoti ya jeshi hilo.
Wanahabari walitaka kujua kauli ya jeshi hilo kufuatia Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA) kutangaza kuwa wamepeleka maombi polisi iwaruhusu kufanya maombi Jumapili ijayo katika Uwanja wa TP Sinza ili wamuombee Tundu Lissu aliyeko Hospitali ya Nairobi baada ya kujeruhiwa kwa risasi.
“Hatutarushusu mkusanyiko wowote usiokuwa na kibali, tunaruhusu sana mtu kufanya maombi katika maeneo maalum yanayotambulika, yapo makanisa, ipo misiskiti na mahali pengine ambapo ni rasmi.
“Hatuwezi kuruhusu mikusanyiko yenye viashiria vya uvunjifu wa amani, kama ni kanisani au msikitini wewe nenda ufanye maombi yako hata kama utakesha na si vinginevyo,” alisema Kamanda Mambosasa.