
JUKWAA la Katiba Tanzania (Jukata) limesema limebaini kwamba baada ya kuifuatilia na kuichambua bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa miaka miwili mfululizo ya mwaka 2016/17 limebaini serikali haijatenga fedha zozote kwa ajili ya ukamilishaji wa mchakato wa katiba mpya wala hakuna maelezo ya kina juu ya hatma ya mchakato huo muhimu.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukata, Hebron Mwakagenda, alisema kuwa hata kama Rais Magufuli hakusema katika kampeni zake kwamba atakamilisha mchakato wa marekebisho ya katiba lakini kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho kinaongoza serikali kilisema kitafanikisha kukamilisha mchakato wa katiba iliyopo, inaonekana kuwa na mapungufu ya kisheria.
“Kutokana na kutotengwa kwa fedha yoyote kwenye bajeti ya serikali kwa ajili ya mchakato huu adhimu, matumaini ya Watanzania wengi yalikuwa kwamba mchakato wa katiba hiyo ungeweza kukamilishwa katika kipindi cha kwanza cha utawala wa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli.
“Sasa matumaini yameanza kufifia kwani katika mazingira yaliyopo, kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kumebaki fursa finyu sana ya kuandaa bajeti ya dharura na kuipitisha katika kipindi hiki cha mwaka 2017,” alisema.
Aidha amelaani kitendo cha kushambuliwa kwa risasi na kujeruhiwa vibaya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, na watu wasiojulikana mjini Dodoma wiki iliyopita.
Amevitaka vyombo vya dola kufanya kazi yake kikamilifu ili wahusika wakibainika wafikishwe kwenye sheria.
Kuhusu uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Kenya Septemba 8 mwaka huu na hatimaye kufutwa na mahakama ya juu ya Kenya Septemba Mosi, alisema hiyo inaonyesha uimara wa katiba ya nchini humo iliyopitishwa mwaka 2010 na hivyo iwe funzo kwa Tanzania kwamba ni muhimu na ni wakati muafaka sasa kwa matokeo ya rais kuhojiwa mahakamani.