






Diwani wa Kata ya Kongowe, Kibaha mkoani Pwani, Iddy Kanyalu amewaasa wahitimu wa kidato cha nne wa Sekondari ya Mwambisi iliyopo Kongowe, kujiepusha makundi ya kihuni baada ya kuhitimu elimu hiyo badala yake wajikite kuwasaidia wazazi wao na jamii, kwa kujishughulisha na ujasiriamali.
Diwani Kanyalu aliyasema hayo wakati wa mahafali ya pili ya shule hiyo yaliyofanyika Alhamisi ya Oktoba 5, 2017 ambapo yeye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi, akawasisitiza wahitimu hao pia kujiendeleza kielimu kwa kusoma kozi mbalimbali wakati wakisubiri matokeo.
Katika risala yao, wanafunzi wa shule hiyo walieleza changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo ambapo Diwani Kanyalu alitoa shilingi milioni moja kwa ajili ya maendeleo ya sekondari hiyo na kuahidi kuzifanyia kazi changamoto alizoelezwa.
“Nafahamu shule hii ni changa na ina changamoto nyingi zinazoikabili lakini najikuna pale ninapofikia, sehemu iliyobaki nitaenda kusaidiana na halmashauri ya mji, nitachangia shilingi milioni moja lakini pia niungane na wazazi hawa katika furaha ya wahitimu hawa 39, nitatoa elfu tano kwa kila mmoja wao,” alisema Kanyalu.
Aidha, Kanyalu amewasisitiza watoto hao kutulia kipindi hiki wakiwa wanaelekea kwenye mitihani yao ya mwisho na kusoma kwa bidii pamoja kwa kuwa serikali ya sasa imefuta karo na kuongeza kuwa wazazi wawahimize watoto wao kupenda shule ili wapate elimu bora itakayowasaidia maishani.
Akizungumza katika mahafali hayo, mkuu wa shule hiyo, Joseph Simba, alisema shule hiyo ina mahitaji ya vyumba 12 vya madarasa ambapo kwa sasa ina madarasa 6 hivyo uongozi wa shule unaomba usaidiwe kuhusu hilo.
“Shule yetu pamoja na changamoto tulizonazo katika upande wa elimu tumejitahidi kupambana, katika kipindi cha miaka mitatu tumeweza kufaulisha kidato cha pili kwa wastani wa A na mwaka uliopita, wanafunzi 9 walifanikiwa kujiunga na kidato cha tano na wengine katika vyuo vya afya na ufundi stadi,” alisema.
STORI : DENIS MTIMA/GPL