×

Dansi Inapita Barabara ya Bongo Movie!

Ally Choki na waimbaji wake.

ACHANA na muziki wa Dansi ile ya zamani, ya bendi kama Marquis, MK Beats, Dar International, Mlimani Park au Juwata Jazz, nazungumzia Dansi hili la kisasa, enzi hizi za akina Twanga Pepeta.

Miaka 10 tu iliyopita, waimbaji wa muziki wa Dansi walikuwa ndiyo mastaa wakubwa mtaani. Kukutana na mtu kama Ally Choki, marehemu Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’ au Muumini Mwinjuma ‘Kocha wa Dunia’, ilikuwa umekutana na mmoja wa watu wakubwa, adimu.

Kukaa meza moja na Nyoshi El Saadat, Jose Mara, Rogart Hegga, Adolf Mbinga, Luiza Mbutu, Jessica Charles, Amina Mnoga ‘Kimobitel’, Hamis Amigolas au Msafiri Diouf ilikuwa ni heshima kubwa, kwa sababu upo na watu ambao wanaiburudisha nchi.

Banza Stone enzi za uhai wake.

Burudani ilipata kushuhudia ‘vita’ vya ukubwa kati ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ na FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma a.k.a Wazee wa Pamba ‘Bling Bling’. Kila kundi lilijiona kuwa juu kuliko mwingine na ushindani wao uliwapa raha mashabiki.

Wakati Twanga iliiteka Jumapili mchana kwa tamasha lao la kila wiki katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Wazee wa Ngwasuma waliifanya siku hiyo kuwa maalum nyakati za usiku, ilipowachukua karibu watu wote waliokuwa wakiburudika huko na kuwahamishia Msasani Club, uwanja wao wa nyumbani.

Lakini haikumaanisha kuwa muziki wa Dansi ulikuwa chini ya bendi hizo tu. Kulikuwa na Mchinga Sound, Akudo Impact na TOT Plus ambazo zilikuwa zinapigana vikumbo kupora ufalme wa wawili hao, kazi yao kubwa ikawa ni kushindana kupora wanamuziki wazuri ili kuimarisha kikosi.

Asha Baraka.

Ndiyo maana Mchinga Sound walitumia fedha nyingi kutengeneza kikosi imara chini ya Mbinga, wakati Aset, walifanya kazi kubwa kumsogeza Kocha wa Dunia kuipaisha African Revolution ‘Chipolopolo’, huku Akudo Impact ikilazimika kuvuka mipaka hadi Kongo DRC kwenda kufanya ‘shopping’ ya wanamuziki na wanenguaji.

Ni muziki huu ndiyo uliipa hadhi sanaa ya uchezaji (unenguaji) kwani uliweza kutengeneza pia mastaa, waliokuwa wakitembea vifua mbele kujivunia kazi yao ya kunengua jukwaani.

Ni wakati ambao ulikutana na marehemu Aisha Madinda, Lilian Internet, Super Nyamwela, Diana Astonvilla, Janet Isinika, Queen Suzy, Aisha Mohamed, Rukia Bruno, Otilia Boniface na wenzao wa enzi hizo.

Nyoshi.

Na tukashuhudia utitiri wa wanamuziki wachanga wakiibuka na kujizolea umaarufu mkubwa. Charles Gabriel ‘Chalz Baba’ alikuwa mchanga wakati akina Choki na Banza Stone wakikamata usukani pale Twanga, lakini alikwenda hadi kuja kuwa kiongozi mkubwa kabisa wa Mashujaa Bendi.

Wakaja akina Khalid Chuma ‘Chokoraa’ aliyezaliwa akitokea Extra Bongo, Kalala Junior, Saulo John ‘Ferguson’ na wenzao wa enzi zao.

Ni kipindi ambacho wakati Mango Garden ilikuwa ikijaza nyomi kwa waumini wa Twanga, Msasani Club ilikuwa ni lazima watu wakeshe ili kufaidi mambo ya wazee wa bling bling huku Akudo Impact ‘Vijana wa Masauti’ chini ya Christian Bella wakikamata hatamu katika fukwe za Msasani Beach Club.

Muziki wa Dansi ulikuwa juu, bendi zikiwalipa wanamuziki wake mishahara mizuri, zikipata mialiko ya kila siku kwenda mikoani na wakifanya shoo za mjini kwa bei mbaya!

Muumini Mwinjuma.

Ulikuwa ni wakati ambao wahusika wa bendi waliweza kusimama getini na kukataa mtu fulani asiingie na anayekatazwa akaweza hata kutoa machozi kwa jinsi anavyokosa burudani.

Ally Choki, Muumini Mwinjuma na Banza Stone, kila mmoja kwa wakati wake waliweza kuanzisha bendi na zikaajiri vijana wengi ambao walifanya kazi kubwa kuhakikisha muziki wa Dansi unaendelea.

Lakini ghafla, muziki wa Dansi umeporomoka kwa kiwango cha ajabu, kiasi kwamba bendi kubwa kama Twanga Pepeta na FM Academia, zinapiga shoo kwa kiingilio cha bia!

Ingawa wenyewe wanadai kuwa hali hiyo hutokea wakati bendi inakuwa imeshalipwa, ukweli unabaki kuwa hadhi ya dansi imeyumba, kwa sababu jambo hili (la kupiga kiingilio bia), lingefanyika miaka mitano iliyopita, lazima kungetokea maafa kwa wingi wa watu ukumbini!

Ni kama ilivyotetereka Bongo Movie, kiasi cha kuwafanya watu kudhihaki kuwa filamu zimeondoka na Steven Kanumba, kana kwamba yeye ndiye alikuwa muasisi.

Sijui nini kimetokea, lakini huwezi kubisha kuwa mvuto wa dansi, hasa jijini Dar es Salaam, umepungua mno. Ally Choki, aliyekuwa kipusa, hivi sasa hawezi tena kumsumbua Asha Baraka kwa sababu hata yeye akiwepo jukwaani, bado mahudhurio ya mashabiki ni yaleyale sawa na anapokuwa hayupo.

Wadau wa muziki huu wanapaswa kukaa chini na kutafakari upya nini cha kufanya ili kuwasogeza tena mashabiki katika kumbi za burudani, kama wanavyojiuliza watu wa

Makala: Ojuku Abraham

Leave a Comment