RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo Oktoba 30, 2017 amezindua kiwanda kipya cha Sayona kitakachokuwa kikichakata matunda na kusindika Juice katika maeneo ya Nyakato jijini Mwanza.
Katika uzinduzi huo, Rais Magufuli ambaye aliambatana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Charles Mwijage, Waziri wa Ujenzi, Prof. Makame Mbarawa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, amewapongeza viongozi hao kwa jitihada zao za kuhakikisha tanzania yenye viwanda inapatikana na kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Aidha Magufuli amewapongeza wamiliki wa kiwanda hicho kwa kusema kuwa serikali yake inawaunga mkono wafanya biashara wote ambao wangependa kujenga viwanda nchini.
“Nawapongeza Subash na wafanyakazi wako, umejenga kiwanda ndani ya nchi badala ya kwenda nje, serikali yangu itawashika kwa mikono miwili, na haya ndiyo maendeleo. Kama umeajiri watu 200, maana yake umesaidia familia nyingi kujikwamua na kufaidi maisha yao,” alisema Magufuli.
Aidha amempongeza Mkuu wa Mokoa, Mongella akisema serikali iliteleza kipindi cha nyuma lakini si wakati mwafaka wa kuanza kulaumiana, hivyo kiongozi huyo amefanya jambo jema la kufufua viwanda na kushawishi wawekezaji kujenga viwanda mkoani humo.
“Huwezi kukaa na kiwanda zaidi ya miaka 20 na huwezi kukiendeleza na sisi tuakuvumilia, tutakunyang’anya tu, Mkuu wa Mkoa nakupongeza kwa kuwanyang’anya kiwanda cha Mwanza Tanneries kilichokuwa kikichakata ngozi, kilitelekezwa lakini umeamua kuwanyanga’anya,” alisema magufuli.