



KATIKA harakati za kuendelea kumlinda na kutetea haki za watoto wa kike, Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Chini ya Udhamini wa Shirika la Maendeleo Sweden (Swedish International Development Cooperative Agency-SIDA) limeelezea mafanikio ya kumlinda mtoto wa kike na namna ya kumfanya ajitambue.
Kongamano hilo limefanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Lamada jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya watoto Wizara ya Afya, Magreth Mussai.
Katika kongamano hilo, watoto washiriki walipata fursa ya kuelezea mafunzo mbalimbali waliyoyapata kutokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya shirika hilo ikiwa ni pamoja na miradi ya kutokomeza ukeketaji, mimba za utotoni, ndoa za utotoni na ukatili wa kijinsia.
”Vijana wakiwa ndiyo mabalozi wa shirika letu wamepata fursa ya kuelezea ni kwa namna gani wanafanya kazi kwa kuelimisha jamii juu ya ukatili wa kijinsia, ukeketaji na mimba za utotoni ili kufikia dhana ya taifa ya kuleta usawa wa kijinsia,” alisema.
Shirika la Utu wa Mtoto (CDF) ni shirikia la hiyari lisilo la kiserikali ambalo lilisajiliwa mwaka 2006 chini ya sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo makao makuu yake yako jijini Dar es Salaam.
Lengo kuu la shirika hilo ni kutekeleza programu na mipango mbalimbali yenye kukuza, kutetea na kuboresha haki na ustawi mtoto wa Kitanzania.
Miongoni mwa washiriki wa kongamano hilo limehudhuriwa na walimu, polisi, maofisa maendeleo na ustawi wa jamii na wasichana walio nje ya shule.