
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina, amesema kuwa, endapo ikitokea wapinzani wao wa jadi, Simba wakateleza, basi waandike wameumia katika suala zima la kuchukua ubingwa msimu huu.
Lwandamina ameyasema hayo baada ya Simba kuwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 22 na kuiacha Yanga kwa pointi mbili ikiwa nafasi ya tatu, huku Azam ikikabana koo na Simba kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Mzambia huyo ameongeza kuwa, licha ya wapinzani wao hao kuwakimbia kila siku, lakini hawataacha kupambana kuona na wao wanashinda mechi zao kuhakikisha hawawaachwi mbali.

“Tunahitaji kutetea ubingwa wetu, bado vita inaendelea na kila siku ushindani unakuwa mkubwa kutokana na kila timu kuhitaji ubingwa, lakini pia hakuna timu ambayo ilikuwa bingwa msimu wa nyuma, kisha ikawa haifikirii kuutetea.
“Wapinzani wetu wanashinda mechi zao, na sisi pia tunahitaji kushinda za kwetu, naamini kwa mwendo tulionao kama tukiendelea kuwa na matokeo mazuri kila siku, basi huko mbele lolote linaweza kutokea,” alisema Lwandamina.
Stori: Omary Mdose | Championi Jumatano