
YANGA wapo kwenye majadiliano ya mwisho kumfuata beki Mrundi, Yusuph Ndikumana anayeichezea Mbao FC ya Mwanza ili imsajili kukiongezea nguvu kikosi chake.
Ndikumana ndiye aliyezuia mipango ya Simba kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara hivi karibuni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza akiwabana vilivyo Emmanuel Okwi na John Bocco wakashindwa kuipa ushindi timu yao na kuambulia sare ya mabao 2-2.
Beki huyo raia wa Burundi, msimu uliopita aliwahi kutakiwa na Simba na Yanga katika usajili mkubwa wa kabla ya kuanza kwa msimu huu, lakini mipango ikavurugika.
Mmoja wa mabosi wa Kamati ya Usajili ya Yanga, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, wamepanga kumsajili beki mmoja wa kati mwenye uwezo na uzoefu wa michuano ya kimataifa ili imtumie katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Miongoni mwa majina yaliyopendekezwa ni Ndikumana huku beki wa zamani wa timu hiyo raia wa Togo, Vincent Bossou, akijadiliwa lakini nidhamu na fedha huenda ikawa kikwazo kwake kurejea tena Jangwani.
“Kama uongozi tumejadiliana usajili wa wachezaji baada ya kupokea mapendekezo ya kocha wetu na kikubwa anahitaji kuboresha baadhi ya nafasi na kati ya hizo ni safu ya ulinzi ya kati ambayo inahitaji beki mmoja mwenye uzoefu wa michuano ya kimataifa.
“Tumeanza mazungumzo na baadhi ya wachezaji na kati yao ni Ndikumana tuliyeshindwa kumsajili katika usajili uliopita, bei ya kumnunua huyu inaweza kuwa chini kuliko Bossou.
“Pia Bossou anayejadiliwa pia huenda asisajiliwe kutokana na nidhamu yake, lakini katika ripoti hiyo ya kocha pia anahitaji mshambuliaji mmoja wa kati ambaye ni mzawa,” alisema bosi huyo.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika kuzungumzia hilo alisema: “Usajili wetu tumepanga kuufanya kiufundi na tunafuata mahitaji ya kocha.
“Tumeanza mazungumzo na baadhi ya wachezaji ambao kocha amewahitaji, tukimaliza kila kitu ndipo tutakapotaja mchezaji anayesajiliwa, hivyo tuachie hapo tu.”
Stori: Wilbert Molandi | Championi Jumamosi