

KAMPUNI ya Msama Auction Mart imesema zoezi la kuwanasa wezi wa kazi za wasanii litaendelea mkoani Morogoro dhidi ya watu wanaodurufu CD feki.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Alex Msama, amesema zoezi hilo sasa linaelekea mkoani Morogoro kuwakamata wezi wa kazi hizo ili wasanii waweze kunufaika na jasho lao kwa kuuza CD zenye stika ya Mamlaka ya Mapato (TRA) ili serikali nayo iweze kunufaika na mapato.
Amesema kuwa si kwamba zoezi hilo limehama katika jiji la Dar es Salaam bali litaendelea kwani kampuni yake imegawanyika katika makundi mbalimbali ili kuweza kuhakikisha kila kona ya nchi watu wanaojihusisha na udurufu kazi za wasanii unapungua.
Ameeleza kwamba zoezi hilo katika mkoa wa Morogoro halitakuwa na siku wala saa na watakaokutwa wakifanya biashara hiyo haramu, sheria zitachukua mkondo wake na watafikisha mahakamani.
“Nawaomba wanaopinga zoezi hili endelevu waache mara moja kwani kufanya hivyo hawataweza kunivunja moyo, mimi nitaendelea kusimamia sheria ya nchi ili serikali na wasanii wanufaike na kazi zao,” alisema Msama.